KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema CCM watazunguka nchi
nzima lakini majibu yatajulikana 2015 kwani ndiyo utakuwa mwisho wao.
Pia
Dk Slaa amesema Chadema hakiyumbishwi na kuahimia CCM kwa waliokuwa
madiwani wake mkoani Arusha, na badala yake kinapata nguvu ya kuweza
kusimamia maadili ya viongozi wake.
Dk Slaa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu
mambo mbalimbali ya kisiasa yanayoendelea nchini, ikiwa ni siku moja
tangu uongozi wa juu wa CCM ukiongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman
Kinana umalize ziara yake ya kwanza katika Mikoa ya Mtwara, Rukwa,
Geita na Arusha.
Alisema Chadema siku zote kitabaki kuwa mwalimu na vyama vingine vitafuata kwa kuiga mambo ambayo chama hicho kimeyaanzisha.
“CCM kuzunguka huku na huko na ni kutuiga sisi kwani tumeanza muda
mrefu, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 tumekuwa tukizunguka na
kuwaeleza wananchi mambo mbalimbali,” alisema Dk Slaa na kuongeza; “Wao
(CCM) wazunguke tu lakini mambo yote yatajulikana 2015 kwani Watanzania
wa sasa siyo wa kudanganywa tena.”
Dk Slaa alisema anashangaa kwa nini CCM wanazunguka huku wakilalamika
wakati wao ndiyo wanaiongoza nchi hivyo majibu ya matatizo ya wananchi
wanayo.“Chadema ni mwalimu na wao hufuata, waendelee na mzunguko wao
lakini waache kulalamika kama sisi bali watoe majibu kwa kuwa wao ndiyo
wanaongoza Serikali,”alisema Dk Slaa.
Akizungumzia baadhi ya madiwani wa chama hicho waliohamia CCM, Dk Slaa
alisema kuwa hawakiyumbisha chama chao na kwamba hata kama wamehama
wasipolipa Sh15 milioni kama amri ya mahakama ilivyotolewa watakwenda
jela.
Juzi katika mkutano wa CCM Arusha, madiwani wa Chadema walitangaza
kujiunga na CCM huku wakipinga hatua ya Dk Slaa, kuwa alikuwa akitaka
kuwafunga baada ya kuwatimua ndani ya chama hicho.
Madiwani hao ambao walitimuliwa na Chadema kutokana kitendo chao cha
kumtambua Meya wa Jiji la Arusha Gaudensi Lyimo wa CCM ni Rehema
Mohamed, Simba Salum wa Kata ya Kati na Frank Joseph Takachi wa Kata ya
Olasiti.
Jana Dk Slaa alisema kitendo hicho kinaonyesha jinsi gani kuna wanasiasa
ambao ni matapeli hapa nchini kwani madiwani hao walikwenda mahakamani
kutaka warudishiwe uanachama wao sasa wamekimbilia CCM.
“Watanzania sasa wanajua aina ya wanasiasa matapeli, kama walienda
mahakamani kuomba uanachama wanahangaika nini,”alisema Dk Slaa na
kuongeza; “Chama hakitayumba na tutaendelea kusimamia maadili ndani
chama kama ilinavyotakiwa.”
Alisema baadhi ya madiwani wameshaanza kulipa fedha ambazo mahakama
imesema, hivyo hao waliokimbilia CCM wasipolipa fedha hizo ndani ya
miezi miwili watakwenda jela kama mahakama ilivyosema.
NCCR wanena
Katika hatua nyingine Chama cha NCCR-Mageuzi kimemtaka Makamu Mwenyekiti
wa CCM, Tanzania Bara, Philip Mangula kushughulikia rushwa ndani ya
chama hicho kwa muda wa siku saba na siyo miezi sita kama alivyoahidi.
Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Faustin Sungura amesema vinginevyo
chama hicho kitawahamasisha wananchi waikatae CCM katika Uchaguzi Mkuu
wa 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sungura alisema wahusika wa
rushwa wanafahamika na ametoa siku hizo kutokana na kuona miezi sita ni
mingi na watendaji wa vitendo hivyo wanafahamika katika chama na
Serikali na kwamba kinachokosekana ni dhamira ya dhati ya kuchagua
viongozi wenye mikono safi.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment