CHAMA Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kuzindua mafunzo ya
operesheni ya vurguvugu la mabadiliko (M4C) yatakayoanza Novemba 22
mwaka huu hadi Novemba 23 katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera. Mafunzo
hayo yatatolewa kwa wenyeviti na makatibu wa vyama hivyo ngazi ya
wilaya hadi mkoa yenye lengo la kuleta uongozi bora na kueneza sera
sahihi ya chama hicho. Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mafunzo
na Oganaizesheni, Benson Kigaila alisema mafunzo hayo yamekuwa
wakifanywa kwa wanachama wao ili kupata mbinu mbalimbali ya kudai haki
na uwajibikaji wa viongozi na wananchi. “Lengo
la kutoa mafunzo kwa wenyeviti na makatibu wa vyama vyetu ni pamoja na
kuwajengea uwezo wa uwajibikaji, kudai haki zao ili kuleta hamasa kwa
Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa mabadiliko, jambo
ambalo linaweza kuwapa matumaini ya maisha,”alisema Kigaila. Aliongeza
kutokana na hali hiyo wanaamini kuwa, mabadiliko hayo yataweza kuleta
uhuru wa kweli na kubadili mfumo wa kiutawala, jambo ambalo litaweza
kuonyesha mafanikio. Alisema
kutokana na hali hiyo, jumla ya watu 64 watashiriki kwenye mafunzo hayo
yakiwamo ya darasani na vitendo ili wajumbe hao waweze kusambaza elimu
hiyo kwa wananchi katika vijiji na vitongoji,jambo ambalo litaweza
kurahisisha ufanyikaji wa mikutano ya hadhara. Alisema
mbali na mafunzo hayo, kutakuwa na mikutano ya hadhara itakayotoa
mwongozo kwa viongozi hao kuonyesha uelewa wao katika mafunzo hayo,
jambo ambalo wanaamini wanaweza kufanikiwa. Kwa
mujibu wa Kigaila, Chadema inatarajia kufanya operesheni ya M4C katika
mikoa 32 na kwamba operesheni hiyo itakuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na
zilizowahi kufanyika nchini kwa sababu tayari baadhi ya wajumbe
watakuwa na elimu ya kutosha kuhusu zoezi hilo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment