Siku ya Oktoba 6 mwaka huu kulifanyika Kongamano la wazi la kujadili
mustakabali wa Zanzibar wakati wa mchakato wa utoaji maoni kuhusu katiba
mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kongamano lile
walipokuwepo wanasiasa vijana wa Zanzibar, wenye kuvuta hisia za wengi,
hao si wengine ni Mansoor Yussuf Himid na Ismail Jussa Ladhu. Lakini
aliyefunika kongamano hasa ni Askofu wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini
Zanzibar Emmanuel Masoud.
Masoud alisema upepo wa mabadiliko hauwezi kurudhishwa nyuma na ikiwa
wazanzibari wanahitaji kupewa fursa ya kuwa huru kwa nini wanazuiliwa
wakati katika dunia ya sasa hakuna kulazimishana katika masuala ya
utawala.
Askofu huo aliwakosha sana washiriki wa kongamano hilo ingawa awali
kama kawaida ya wazanzibari ambao silimia kubwa ni waislamu wamekuwa na
shaka juu ya wenziwao wakristo wakiamini kila mkiristo ni mtetezi wa
Muungano lakini hali isivyotegemewa alipopanda jukwaani na kukamata
kiriri Askofu Masoud alishangiriwa baada ya kuungana na wazanzibari
wenzake na kudai Zanzibar huru kitaifa na kimataifa.
“Ni Jambo la ajabu sana kuona wazanzibari wakitaka kuwa na nchi yao
halafu wasipewe ….wazanzibari wana madai yao ya msingi na hivyo lazima
wasikilizwe na wasiposikilizwa tunaweza kuingia katika matatizo kwani
wakati umefika Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili” alisema Askofu
Masoud na kushangiriwa na ummati mkubwa uliofurika katika ukumbi huo.
Ingawa kila mchangiaji alipewa dakika kumi lakini dakika chache hizo
watoaji mada walizitumia vyema ili kukidhi haja ya ukumbi ambapo baada
ya kujitambulisha Askofu alijiita yeye ni Mpemba na anatambulika hivyo
pale kanisani Mkunazini kwani yeye alizaliwa Pemba na hivyo kuzidi
kuvuta hisia za wazanzibari wengi waliopo pale katika kongamano.
Watu wengine waliongara katika kongamano hilo wakawa ni wanasiasa
hawa ni wanachama wa vyama tofauti, Mansoor CCM na Jussa CUF, lakini
wanaunganishwa na uzalendo wa kizanzibari juu ya nchi ya uzao wao. Na
licha ya hoja zao wanazotoa lakini wameweza kuwavuta wazanzibari wengi
katika medani za siasa wakiwemo watu wa rika tofauti.
Aliyeanza kufungua dimba ni Mansoor ambaye aliwataka wazanzibari
kutokuwa wepesi kuwanyooshea vidole wao kwa wao kwa sababu ya tofauti
ya mawazo juu mfumo wa muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mansoor aliwataka wazanzibari na hasa vijana kuzungumza kwa uwazi na
tena bila ya woga hasa katika mustakbali wa nchi yao katika Muungano.
Alishangazwa na baadhi ya wanasiasa tena wengine ni viongozi wakubwa
wanaosimama na kusema hadharani kuwa “mkiutaka msiutake Muungano ndio
huu huu” kuwa wanakosea kwani hakuna mwenye haki ya kumlazimisha mtu juu
ya anachokitaka mwenyewe.
“Iweje leo baadhi ya viongozi wawatishe wananchi juu ya mustakbali wa
nchi yao” Alihoji huku akishangiliwa na umati uliosheheni ukumbi wa
salama pale Bwawani Hotel.
Pengine hoja ya mwanasiasa huyu ni kuwa Wazanzibari wanahitaji umoja
zaidi kuliko kitu chengine chochote hususan katika wakati huu wa
mchakato wa maoni ya Tume ya Jaji Wariona juu ya katiba mpya.
Je, Mpaka lini Wazanzibari tutakubali kugawiwa. Kwa nini viongozi
wetu wa kisiasa badala ya kuweka maslahi ya Zanzibar mbele, wao wanaweka
mbele maslahi yao au maslahi ya vyama vyao? Hayo ndio yalikuwa maneno
ya Mansoor bila ya kuyatafuta na akaongeza kwamba.
“Msiogope kusema wala kuondoshwa katika nafasi zenu ikiwa umakamu wa raia utaupata tu ….” alisema bila ya kutafuna maneno.
Mansoor ambaye wakati huo alikuwa ni waziri ambapo sasa ameondoshwa
katika wadhifa wake huku sababu kubwa ikidaiwa ni kauli yake aliyoitoa
katika kongamano hilo lililofanyika Bwawani Hoteli na kurushwa moja kwa
moja na baadhi ya vyombo vya habari nchini.
Alisema inafaa Wazanzibari tukaelewa kuwa huu si wakati mwafaka wa
kupingana wenyewe kwa wenyewe. Huu si wakati wa kutazama maslahi ya mtu
binafsi wala chama! Ni wakati wa kutazama maslahi ya Zanzibar kwanza na
mustakabali wa Wanzanizbari.
Tuacheni tabia ya kushughulikia mambo madogo madogo ambayo hayana
manufaa kwetu wala kwa kizazi chetu, twendeni pamoja katika yale mambo
ya msingi kama hili la kutaka mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano.
Rais wa awamu ya pili Zanzibar, Al-Hajj Aboud Jumbe Mwinyi
alilazimishwa ajiuzulu uongozi kwa kudai serikali tatu. Na baadhi ya
Wazanzibari walisherehekea kufukuzwa kweke. Lakini Rais wa Zanzibar,
aliyechaguliwa na Wazanzibari kwa kura anakuja kuondoshwa madarakani na
kikao cha CCM cha NEC chenye wajumbe kiasi cha 200 tu! Niajabu!
Wazanzibari hawalioni hilo.
Umefika wakati Wazanzibar tuache jazba, tuache ubinafsi, vyama vyetu
tuviweke kando na tuungane katika kupigania maslahi ya Zanzibar ndani
ya Muungano. Hakuna anayepinga muungano, lakini tunapinga kuburuzwa na
mfumo dhaifu wa muundo uliopo ambao unaifanya Zanzibar kuwa kama mgeni
mwalikwa katika Muungano.
Ndipo akina Mansoor walipoeleza kwa kina ulazima wa kuvumiliana
katika tofauti ya mawazo, tofauti ya itikadi ya kisiasa, lakini pia
katika madai ya haki za Zanzibar na mustakabali wake suala hilo halina
dini, halina siasa wala kiongozi, kila mmoja anawajibu na haki.
“Si kila lililozungumzwa hapa mkakubaliana nalo, wapo wanaotofautiana
nami, lakini nanyi mnapaswa kuwavumiliana wengine ambao hawatakubaliana
na mawazo yetu, kwa hivyo tuheshimu haki ya kila mmoja,tuheshimu sheria
na tutumie busara zaidi kuliko kutawaliwa na hisia za kijazba” alisema
Mansoor.
Anazungumziaje kuhusu mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Jakaya Kikwete katika kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar?
“Kwa hakika mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi na Rais wetu wa
Jamhuri ya Muungano, anastahiki kila aina ya pongezi na sifa kwa
ushupavu wake kushughulikia mpasuko wa kisiasa Zanzibar”
Mansoor anamtaja Rais Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi mkweli, makini,
jasiri na mwenye upeo mkubwa akiwa ndio muasisi wa maridhiano ya
kisiasa Zanzibar hadi kufanikiwa kwake na leo Wazanzibari wanaishi kwa
amani na kuheshimiana.
“Kati ya Marais wote waliopita ni yeye aliyethubutu kusema hadharani
tena kwa kichwa kipana kwamba anasononeshwa na mpasuko wa kisiasa
Zanzibar na kuahidi kuutafutia dawa, kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa
yaliyohitimishwa kwa kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni juhudi zake
Rais Kikwete,Waziri Mansoor aliwakumbusha washiriki wa Kongamano la
wiki iliyopita.
Hakuwa Waziri Mansoor bali washiriki wa kongamano nao hawakufanya
khiyana kumwagia sifa Rais Kikwete kwani amekuwa mkweli wa ahadi yake ya
kuheshimu haki za binadamu na amekuwa na dhamira ya dhati kuimarisha
uhuru wa Watanzania.
Wanakongamano wamesema kitendo cha Rais Kikwete kukubali mchakato wa
katiba mpya,viongozi wa kisiasa hususan wale wa CCM wanapaswa
kumheshimu Mwenyekiti wao na kuwaachia wananchi kutoa maoni yao bila
vitisho na masharti kwani hatuwezi kupata katiba na mfumo wa muundo
Muungano iliyoridhiwa na Wazanzibari wote.
Wanasema kinyume chake tutaendelea kuwa na mfumo wa Muungano
usiotakiwa. Wazanzibari wale kike kwa kiume wakasisitiza kwamba uhuru
mpana wa kutoa maoni utaleta hali halisi hiyo itawapa fursaviongozi wa
kisiasa kufanya maamuzi sahihi kwa niaba ya wananchi hali ambayo
itaimarisha Muungano wetu.
Waziri Mansoor akasema ipo haja ya kuwa na Muungano wa mkataba ili
kuondokana na malalamiko mengi ambayo yanalalamikiwa katika mfumo wa
muundo wa sasa wa Muungano na kusisitiza bado ataendelea kuwa muumini wa
mfumo wa Serikali mbili chini ya muundo wa Muungano wa mkataba mfumo
ambao utaipa fursa zaidi Zanzibar kujijenga na kujitegemea kiuchumi.
Mzee Hassan Nassor Moyo hakuwa nyuma katika kongamano hilo kwani ni
yeye aliyeanza kufungua dimba kwa kueleza kwanini leo anataka mabadiliko
ya mfumo wa muundo wa Muungano, anasema mfumo wa sasa hauwezi kukidhi
haja ya kizazi za leo na cha baade hivyo kuna haja ya kukubali
mabadiliko ya mfumo kwa kuwa na Muungano wa mkataba baina ya Tanganyika
na Zanzibar.
Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Salim Rashid
akasema kwa uelewa wake ni kwamba mazingira ya wakati ule ya kuundwa kwa
Muungano yalikusudiwa kuidhibiti Zanzibar kwani Mataifa ya nje hasa ya
Magharibi yalikhofia Zanzibar kugeuka Cuba ya Afrika.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa yeye ameungana na
wasemaji wengine waliomtangulia, lakini alitoa angalizo la Tume ya Jaji
Warioba inayokusanya maoni ya wananchi kutofanya kinyume na matakwa ya
Wazanzibari watakavyotoa maoni yao.
Jussa alisema maoni ya Wazanzibari hayana budi kubaki kama
yatakavyotolewa katika mikutano ya Tume na kwamba ikiwa kutakuwa na
uchakachuaji basi wajumbe wa Tume waelewe kuwa watabeba dhima mbele ya
Mwenyezi Mungu.
Kimsingi wengi wanakubali kwamba kongamano lile limetoa picha ya hali
halisi ya hisia za Wananchi kutaka mabadiliko ya mfumo wa muundo wa
Muungano wakitaka uwepo ule wa mkataba badala ya huu wa kikatiba ambao
hautoi fursa sawia kwa Zanzibar kujiamulia mambo yake wenyewe kama
kuingia mikataba ya kimataifa na mambo mengine.
Hata hivyo, wapo baadhi ya watu ambao hawaungi mkono vuguvugu la
mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano, hawa wanasimamia nguzo za
vyama vyao si utashi wao wala hisia zao,bali wanaongozwa na sera za
vyama vyao vya siasa hata kwa mfano vyama vyao vikiwaelekeza sipo wao
watafuata ilimradi ni Chama kinachotaka.
Siku za mwanzoni mwa harakati za madai ya wanamageuzi hawa ndio
waliokuwa wakitamba kwamba wao ndio wanahaki zaidi na wana uchungu
zaidi na nchi hii kuliko Wazanzibari wengine. Kwa tafsiri nyengine ni
kwamba hawa hawachelewi kuyaelekeza mambo kule wanapopataka wao hata
kama ni kinyume na hali halisi.
Nimeandika sana huko nyuma kwamba suala la mfumo wa muundo wa
Muungano sio la Vyama vya siasa maana zilizoungana ni nchi mbili
huru,iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
ndizo zilizoingia mkataba wa kuunganisha Mataifa yao iweje leo hoja ya
mabadiliko ya muundo wa Muungano iwe ya vyama vya siasa?
Waumini wa demokrasia wanaamini vitendo vya viongozi wa kijamii
katika nafasi yoyote ile kinatakiwa kudhihirisha matakwa ya wananchi na
sio yale matakwa wanayoyataka wao?
Nguzo muhimu ya demokrasia ya kweli ni pamoja na kuvumiliana katika
maoni tofauti ya kisiasa na kwamba maoni ya kisiasa ya wananchi ni
lazima yasikilizwe na haki zao za msingi kuheshimiwa?
Baadhi ya watu wanadhani kwamba wao wakisema chochote, hicho ndio
huwa ‘sadakta’, lakini akisema mwingine asiye ‘mwenzao’, huyo hupewa
majina ya kumkosanisha na jamii, watampakazia kuwa yeye “msaliti,
Hizbu-ZNP, mchochezi” hakitakii mema Chama, “anataka kuvunja Muungano,
msaliti wa Mapinduzi, anachanganya dini na siasa” na mengineyo.
Chanzo: Mzalendo.net
No comments:
Post a Comment