Na Rajab Ramah, Nairobi
Wasiwasi unaongezeka juu ya uwezo wa vikosi vya usalama vya Kenya
kuzuwia vurugu na kujibu matatizo kwa ufanisi huku uchaguzi mkuu ukiwa
umebakia miezi mitatu tu, vikundi vya asasi za kiraia vyasema.
Afisa
wa Kitengo cha Huduma Maalumu akimpiga teke kijana wa kenya katika
kitongoji cha Eastleigh Nairobi hapo tarehe 19 Novemba, siku moja baada
ya bomu kulipuka katika basi dogo, lililowaua watu saba. [Na Carl de
Souza/AFP]
Tabia za polisi hivi karibuni katika kukabiliana na vitisho vya usalama
zimezua hofu na wasiwasi kuliko uhakika miongoni mwa wananchi, kwa
mujibu wa Odhiambo Oyoko, mratibu mtendaji wa Kituo cha Uimarishaji Haki
na Ulinzi.
"Kila operesheni ya polisi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu
huishia katika kukamata watu kwa makundi bila ya kuchagua, ubakaji,
uvamizi, au aina nyengine ya vurugu [zinazoelekezwa] kwa watu wasio na
hatia. Hili ni kinyume na dhamiri ya kupambana na uhalifu," alisema,
akikisudia operesheni za karibuni huko Tana River Delta, Baragoi,
Eastleigh na Garissa.
Mwezi wa Septemba, zaidi ya watu 100 waliuawa katika mapambano ya
kikabila huko Tana River Delta, wakiwemo maafisa wa polisi tisa, kabla
ya vikosi vya usalama kuweza kuidhibiti hali hiyo.
Tarehe 10 Novemba, polisi 42 waliuawa na majambazi huko Baragoi Wilaya
ya Samburu katika Mkoa wa Bonde la Ufa. Kutokana na madai kuwa polisi
walichukua hatua kwa taratibu katika kushughulikia mzozo huo, Rais wa
Kenya Mwai Kibaki alipeleka Vikosi vya Ulinzi vya Kenya katika eneo hilo
ili kuwasaidia polisi.
Siku tisa baadaye, kuuliwa kwa risasi askari watatu wa Vikosi vya Ulinzi
vya Kenya huko Garissa kulipelekea maafisa wa jeshi kulipiza kisasi kwa
jamii katika ghasia za utumiaji nguvu.
Kukosekana na uratibu, polisi wenye zana hafifu
Simiyu Werunga, mkurugenzi wa Kituo cha Afrika cha Masomo ya Usalama na
Mikakati kilichoko Nairobi, alisema kuwa hadithi kama hizo zimekuwa za
kawaida sana katika miezi ya karibuni, na mara nyingi mashambulizi ya
kigaidi ndio huifanya hali kuwa mbaya zaidi.
Werunga, kapteni wa jeshi mstaafu, alisema kukosekana kwa uratibu
miongoni mwa vyombo vya usalama ndio sababu ya kuendelea kukosekana kwa
usalama.
"Tumeona kesi ambapo jeshi au Kitengo cha Huduma Maalumu kinapelekwa ili
kushughulikia kutokuwepo kwa usalama, ambapo polisi wa kawaida
wangeweza kuidhibiti hali hiyo," aliiambia Sabahi. "Hali hii unazua
mtafaruku na kuleta hofu kwa umma."
Alisema kuwa hatua madhubuti za usalama zinapasa kuchukuliwa mara moja
ili kuwahakikishia Wakenya uchaguzi wa amani na salama hapo tarehe 4
Machi 2013.
"Kuna haja ya kuwa na mkabala ulioratibiwa vyema ambao utavijumuisha
vyombo vyote katika kugundua na kushughulikia uhalifu," alisema. "Hii
inaweza kutokea iwapo vitengo vyote vya polisi vimewekwa chini ya
uongozi mmoja wa mkoa."
Polisi wanapaswa kuacha kutoa adhabu za kubambikiza kwa wenyeji wa
maeneo ya uhalifu, alisema. Badala yake, wanatakiwa wajenge mahusiano na
jamii ambazo badala yake zinasaidia kutoa intelijensia yenye thamani
ambayo itapelekea kukamatwa kwa wahalifu.
Alisema kuwa ghasia za karibuni za askari huko Garissa na operesheni
zisizochagua zinazowalenga watu wa jamii ya Wasomali katika kitongoji
cha Eistleigh huko Nairobi kumemomonyoa mafungamano na uaminifu baina ya
polisi na jamii.
Philip Onguje, mratibu wa Jukwaa la Mageuzi ya Usalama, kikundi cha
kijamii ambacho kinatetea mageuzi ya sekta ya usalama nchini Kenya,
aliiambia Sabahi kuwa polisi wana zana hafifu za kuweza kushughulikia
miendo inayoibuka ya uhalifu.
Alisema iko haja ya kuwafunza upya polisi katika kudhbiti mizozo ya
uchaguzi na udhibiti wa makundi ili kuepuka matumizi ya nguvu kupita
kiasi au operesheni za usalama zinazopendelea au kuonea upande mmoja.
Onguje alisema kuwa utafiti uliofanywa na jumuiya yake mwezi uliopita
zilionesha kuwa hakuna hata kituo kimoja cha polisi nchini kati ya vituo
456 kina vifaa vya usalama au uwezo wa kupambana na uhalifu.
"Lilipaswa kuwa suala la kumshughulisha kila Mkenya," alisema. "Lazima
sote tushinikize kwa kuwepo kwa marekebisho, kuvipatia vituo vya polisi
vifaa na kuajiri maafisa wengi zaidi wa polisi ndani ya miezi michache
iliyobakia ili waweze kuhakikisha uchaguzi wa salama mwaka ujao."
Serikali inashughulikia kasoro
Kaimu Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani Mutea Iringo aliiambia Sabahi kuwa
serikali inashughulikia wasiwasi huu na inao udhibiti wa usalama wa
nchi.
Alisema kuwa serikali inakusudia kuwapa mafunzo maafisa polisi 7,000
ambao watapelekwa nchini kote ifikapo mwezi Januari ili kuliongezea
nguvu jeshi la polisi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013.
"Pia tutawapa mafunzo maafisa wote kwa uchaguzi, haki za binadamu na
masuala mengine ya kipolisi na tunawahakikishia Wakenya kuwa katika
uchaguzi ujao tutalindwa vyema na maafisa wetu," Iringo alisema.
Serikali pia imo katika mchakato wa kumajiri Inspekta Jenerali wa polisi
katika juhudi za kuhamisha uongozi na kusaidia kupanga upya jeshi zima
ili liweze kukabiliana na uhalifu kwa ufanisi, alisema.
Chanzo http://sabahionline.com
No comments:
Post a Comment