Tamko hilo limo kwenye taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkurugenzi wa
Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare, iliyotolewa jana jijini Dar es
Salaam.
Katika andiko hilo, walimtaka Rais Kikwete atekeleze mambo yaliyoandikwa
kwenye barua ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyetaka
serikali ifanye uchunguzi wa matukio ya utesaji yaliyofanywa na vyombo
vya dola dhidi ya wanaoipinga serikali.
Waraka huo ulitaka uchunguzi ufanyike dhidi ya polisi waliotumika
kuteka, kutesa na kuua kwa malengo ya kisiasa ya kupambana na wakosoaji
wa chama tawala na serikali yake.
Katika taarifa yake, Chadema ilisema walimwandikia Rais wakitaka
kufanyike uchunguzi huru kwa kuunda Tume ya Kimahakama/Kijaji ili ukweli
ujulikane na haki ionekane ikitendeka badala ya kutoa lugha ya kisiasa
kwa nia ya kujikosha mbele ya umma, wakati CCM na polisi, wanakaa na
kupanga mikakati inayopelekea kudhulumu haki na roho za Watanzania.
Aidha, wakati uchunguzi huo ukifanyika, watuhumiwa wote, wakiwemo
viongozi wa CCM, serikali na watendaji wa Jeshi la Polisi waliokubali
kutumika, hata kuvunja haki za binadamu, katiba na sheria, wanawajibika
kwa wao kujiuzulu au kufukuzwa kazi.
Rwakatare alisema kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete
kuwataka viongozi na wanachama wa chama hicho waache kutegemea Jeshi la
Polisi katika kukabiliana na wapinzani ni ushahidi wa tuhuma ambazo
Chadema imekuwa ikitoa dhidi ya chama hicho.
Hivi karibuni Rais Kikwete, alikitahadharisha chama hicho kuwa
kikitegemea zaidi polisi kwamba ndiyo msaada kwake katika kujibu mapigo
ya wapinzani kitashindwa.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Nane CCM baada ya kuchaguliwa kwa
mara nyingine kuwa Mwenyekiti kwa miaka mingine mitano, alisema viongozi
wa CCM lazima wajipange na kuwa wepesi wa kujibu mapigo ya wapinzani.
Alisema jawabu la siasa siyo polisi bali ni wanasiasa wenyewe na kwamba
polisi hawawezi kuwa jibu la suala la siasa lazima kila kiongozi
ajitambue yeye mwenyewe ndiyo mwenezi katika eneo lake.
Chadema ilisema Watanzania wanajua kuwa matukio ya vyombo vya dola
kuhujumu wapinzani na wakosoaji wa serikali ya CCM, kwa nia ya kuilinda
CCM, yamekwenda kwa sababu watu na makundi ya kijamii pia wameanza
kuandamwa.
“Mtu, watu au makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yanaonekana kutoa
mawazo mbadala, kudai haki na uwajibikaji yameanza kuandamwa. Mifano
mizuri hapa ni kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi na kutekwa na kuteswa
kwa kiongozi wa madaktari, Dk. Steven Ulimboka. “ ilisema taarifa ya
Rwakatare.
Chadema ilisema ukweli huo umesaidia kumaliza fumbo lililokuwepo juu ya
madai ya muda mrefu kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa na viongozi
wa CCM na watendaji wa serikali.
“Kauli hiyo ya Kikwete imetufikisha kwenye kilele cha ushahidi kuwa
Jeshi la Polisi linatumika kisiasa kukabiliana na hoja na shughuli
halali za kisiasa zinazofanywa na Chadema , chama mbadala kwa sasa
kinacholenga kuiondoa CCM madarakani”.
Aidha imesaidia kufumbua fumbo la kwa nini Jeshi la Polisi Mkoani Iringa
lilitumia nguvu kubwa kuingilia shughuli halalli za Chadema kufanya
mikutano ya ndani, ikiwemo ufunguzi wa matawi katika Kijiji cha Nyololo,
mkoani Iringa, na hatimaye kusababisha kifo cha Mwanandishi wa Habari,
Daudi Mwangosi, Septemba mwaka huu.
chanzo : NIPASHE
No comments:
Post a Comment