Pages


Photobucket

Sunday, November 25, 2012

Viongozi wa Halmashauri wazomewa mbele ya Nahodha


                      Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha

ZIARA ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha Mkoani Mbeya, imegeuka shubiri kwa viongozi wa Halmashauri za wilaya za Mbozi na Momba, baada ya kujikuta wakizomewa na wakazi wa mji wa Tunduma.

 Tukio hilo lilitokea juzi  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Tunduma, baada ya Waziri kuuliza iwapo wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakipata mikopo ambayo hutolewa na Serikali kama ruzuku kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake na vijana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, ambaye hata hivyo aliwakilishwa na Ofisa Kilimo wa wilaya, Richard Cylili alisema hawatoi fedha hizo kutokana na wasiwasi kwamba wakopeshwaji hawatarudisha.

Jibu hilo lilizua tafrani baada ya wakazi walimiminika kwenye mkuatno huo kuanza kuzomea na kusema kuwa anachosema ni uongo.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu wa CCM (NEC) wa wilaya ya Momba, Jackson Mbwile aliawawshia moto viongozi wa halmashauri baada ya kupanda  jukwaani na kuweka bayana kuwa hakuna kiasi chochote kilichotolewa na Halmashauri hiyo kwa lengo la kuwakopesha wanawake na vijana.

 “Ukweli ni kwamba majibnu yaliyotolewa hapa ni uongo mtupu kwani kama ni suala la watu kushindwa kurudisha mikopo si la kweli kwa kuwa hata mimi ningeweza kuwadhamini na wakafanya vizuri,” alisema Mbwile.

Baada ya kuona hali si shwari Nahodha aliingilia kati kwa kuwaambia wananchi hao wawe  wasikivu kwa kuwa Serikali ya CCM  ni sikivu na ipo kwa ajili ya wananchi.

Aliwaahidi kwamba Serikali itahakikisha inatatua kero hiyo na  kujenga misingi bora ya kuwapatia wananchi huduma, ikiwepo mikopo.
 Hata hivyo aliendelea na jitihada zake za kuwapoza wananchi hao walioonekana kuwa na jaziba kwa kuwaeleza kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha za ruzuku kwa ajili ya mikopo kwa wanawake na vijana ambapo ni jukumu la viongozi katika halmashauri kuzitoa kwa walengwa.

Alisema mbali na ruzuku hiyo, lakini pia Halmashauri zinapaswa kutenga asilimia tano ya fedha za bajeti ya makusanyo yake ya  ndani kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake na vijana ili viweze kujianzishia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbali na Mkurugenzi huyo kuzomewa mbele ya waziri, wengine waliokumbwa na sakata hilo ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Mji  wa Tunduma, Aidan Mwashinga na Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya, Rogasian Shirima.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa mji wa Tunduma, wananchi ambao ni wafanyabiashara walilalamikia kitendo cha Mkurugenzi huyo kuwalazimisha kutoa ushuru mara mbili katika biashara ya samaki ambao huwatoa Mkoani Mwanza na kuwauza Jamhuri ya Demkrasia ya Kongo (DRC).

Waliwalalamikia viongozi wa TRA kwa kufanya kazi zao kwa ubabe, ikiwemo kukamata hovyo bidhaa na kuwalipisha faini kubwa zisizo na uwiano na biashara zao.

Kutokana na kero hizo, Waziri Nahodha aliwaonya watendaji hao na kuwataka wabadilike kwa kuwa chuki hizo zikiendelea zitaendelea kuipaka matope CCM.

Hata hivyo baada ya mkutano huo kufungwa wananchi hao waliendelea kupiga kelele huku wakimtaka waziri huyo kuondoka na viongozi hao kwa madai kuwa hawana tija kwao.

No comments:

Post a Comment