SASA ni
dhahiri sumu aliyoimwaga Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na
makada wengine wa chama hicho mjini Moshi wiki iliyopita, imeanza
kukitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jimbo la
Moshi Mjini, limekuwa likishikiliwa na kambi ya upinzani tangu uchaguzi
wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, huku Chadema kikiigaragaza CCM
katika kiti cha ubunge mara tatu mfululizo.
Makada wa
CCM wamejitokeza na kuhoji ukimya huo wa CCM wakati sumu hiyo imeanza
kusambaa kwa kasi miongoni mwa wananchi na kukiweka chama hicho
njiapanda uchaguzi mkuu 2015.
Kada wa CCM,
Ramadhan Mwindad ‘Gadaffi’ jana alizua kizaazaa katika ofisi za CCM
Moshi Mjini, alipoamua kujitoa mhanga na kwenda kuwahoji viongozi sababu
za kutojibu mapigo. Tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi,
lilisababisha kada huyo na kiongozi mmoja wa CCM ngazi ya wilaya
kushindwa kujibu hoja na kudai kada huyo ametumwa na Chadema.
Kwa mujibu
wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea mbele ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa
CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo
ambaye pia ni Diwani, Michael Mwita.
“Mimi ni
kada wa CCM nimekwenda pale saa 8:00 mchana huu (jana) na kuwauliza kwa
nini kila siku mnafanya vikao vya ndani vya kikatiba, lakini hamwendi
kwa wananchi kujibu mapigo?”alisema.
Badala yake,
kada huyo alisema kiongozi huyo ngazi ya wilaya alimjia juu na
kumtuhumu kuwa ametumwa na Chadema kuhoji mambo hayo na kukwepa kabisa
kujibu hoja ya msingi.
“Viongozi wa
kitaifa wametukanwa na kudhalilishwa sana.Mkuu wetu wa mkoa mpaka
imefikia mahali ameitwa ki model (mwanamitindo) bado viongozi wetu
wamekaa kimya,”alisema.
Kauli hiyo
iliungwa mkono na kada mwingine wa CCM Kata ya Longuo, ambaye alisema
baadhi ya viongozi walijinadi kwa mbwembwe katika uchaguzi uliopita
lakini sasa wanachama hawaoni makeke yao.
“Kuna
viongozi walijinadi kwa wapiga kura kuwa oooh hili ni jembe mchagueni,
mbona kimya? Hata kujibu tu matusi na kejeli za mkutano ule wa Chadema
wameshindwa”alisema kada huyo. Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Elizabeth
Minde alipoulizwa jana kuhusu madai ya wanachama wake alisema yuko
kwenye kikao na pindi atakapomaliza tu angelipigia gazeti hili kutoa
ufafanuzi.
Hata hivyo,
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Mwita alipoulizwa kuhusu tafrani hiyo
alisema hakuona kama kulikuwa na mabishano katika ofisi hizo za CCM kwa
kuwa alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio.
“Nilimwona
Gadaffi na (jina la kiongozi wa wilaya) wakizungumza ila sikujua
wanazungumzia nini, lakini nataka ifahamike CCM ina utaratibu wake wa
kuitisha mikutano na hatujibu matusi,” alisema.
Mwita
alisisitiza kuwa kamwe CCM haiwezi kujibu hoja kwa kusukumwa na mikutano
ya Chadema bali watafanya hivyo kunapokuwa na hoja na CCM iko katika
mchakato wa kujibu mapigo.
Katika
mkutano huo, Dk Slaa, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche
walimwaga sumu inayokifanya CCM kuweweseka.
Katika
mkutano huo viongozi hao pamoja na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema
wanadaiwa kutumia maneno makali kumshambulia Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Leonidas Gama.
Viongozi hao
wa Chadema waliwachongea Gama, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi,
Bernadette Kinabo na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ibrahim Msengi kuwa
wanaingilia utendaji wa Halmashauri.
Kauli za
viongozi hao zilitokana na hotuba ya Meya wa Manispaa ya Moshi
kuwashtaki viongozi hao wa serikali ya CCM kuwa wanazuia utekelezaji wa
maamuzi ya baraza kwa masilahi ya kisiasa.
Meya huyo
alisema viongozi hao wamekuwa wakitumia vibaya vikao vya ushauri mkoa
(RCC) na vile vya wilaya(DCC) kuingilia uamuzi halali wa Manispaa ya
Moshi inayoongozwa na Chadema.
Alitoa mfano
wa viongozi hao kumwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bernadette
Kinabo kuendesha operesheni dhidi ya wafanyabiashara wadogo ili
kuichonganisha Chadema na wananchi.
Kwa mujibu
wa Meya huyo, Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limekuwa katika
wakati mgumu kutokana na Kinabo kukataa kutekeleza maazimio ya vikao
halali ili tu kuinufaisha CCM kisiasa.
Mathalan
alisema, sera ya Chadema Moshi Mjini ni kuwalipia ada wanafunzi wote wa
sekondari ambao wazazi wao hawana uwezo, lakini mkurugenzi huyo amekataa
kuidhinisha fedha hizo.
Meya huyo
alisema mwaka 2011/2012, Halmashauri hiyo inayoongozwa na Chadema
ilitenga Sh196 milioni kulipa ada hizo na mwaka 2012/2013 imetenga Sh216
milioni ambazo zote hazijaidhinishwa.
“Ukimuuliza
anasema sera ya elimu bure siyo sera ya Serikali.Tunaomba hoja hiyo
uipeleke bungeni tujue ni wakati gani vyama vinaweza kutekeleza sera
zake kwa halmashauri inazoziongoza,”alisema.
Meya huyo
alisema vitendo vinavyofanywa na viongozi hao wawili ni dhahiri vina
lengo la kuidhoofisha Chadema kisiasa katika Jimbo la Moshi na pia
kuwagombanisha na wananchi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment