BAADHI ya vigogo wa kisiasa hawatasahau yaliyowapata mwaka jana kutokana
na mabadiliko makubwa yaliyoigusa medani hiyo na kusababisha kuanguka
ama kwa kura au kung’olewa katika nafasi walizokuwa wakizishikilia.
Wakati
baadhi wakiugulia kwa machungu hayo, kwa upande mwingine lipo kundi la
wale wanaosherehekea neema iliyowajia mwaka huohuo, baada ya nyota zao
kung’ara kisiasa na kujikuta wakikwaa nafasi za uongozi, pengine ambazo
hawakuzitarajia.
Miongoni mwa matukio yaliyowatikisa wanasiasa ni hatua ya Rais Jakaya
Kikwete kupangua Baraza la Mawaziri, kutenguliwa kwa baadhi ya matokeo
ya chaguzi za wabunge na uchaguzi wa ndani wa CCM ambao uliwaweka kando
baadhi ya vigogo wa chama hicho.
Kadhalika, yapo matukio yenye sura ya kipekee ambayo yanawagusa
wanasiasa kama Godbless Lema ambaye alianguka kisiasa kwa ubunge wake
kutenguliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha mwanzoni mwa mwaka jana,
lakini akaibuka tena shujaa baada ya kurejeshewa nafasi hiyo na Mahakama
ya Rufani, Desemba 2012.
Tukio kubwa ambalo lilitikisa siasa za Tanzania ni lile la mabadiliko
katika Baraza la Mawaziri ambayo yaliwaweka kando mawaziri sita ambao
walikuwa wakiziongoza wizara nyeti zinazosimamia rasilimali za nchi na
huduma za afya na uchukuzi.
Waliong’olewa ni Mustafa Mkulo (Fedha), William Ngeleja (Nishati na
Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (Uchukuzi), Dk
Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Haji Mponda (Afya na Ustawi wa
Jamii). Pia panga hilo liliwakumba waliokuwa Naibu Mawaziri, Dk Lucy
Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).
Kuanguka kwa Mkulo, Ngeleja na Maige kulitokana na taarifa ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyozihusisha wizara zao na
ufisadi. Dk Mponda na Dk Nkya, waling’olewa kutokana shinikizo la
madaktari ambao walifanya mgomo uliotikisa sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake, Nundu naibu wake, Dk Mfutakamba waling’olewa kutokana
na kashfa ya ujenzi wa gati bandarini ambao uliwagawa kiasi cha
kutofautiana bungeni, wakati Dk Chami naye aliponzwa na ugomvi na
aliyekuwa naibu wake, Lazaro Nyalandu. Hata hivyo Nyalandu alipona baada
ya kuhamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walioula
Mabadiliko hayo yalikuwa neema kwa wateule wapya wakiwamo wale ambao
hawakuwahi kuwa wanasiasa kama ilivyo kwa Profesa Sospeter Muhongo
ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Profesa Muhongo alipewa naibu wawili; George Simbachawene (Nishati) na Stephen Masele (Madini) ambao walikuwa wabunge.
Wabunge wengine walioula ni Dk William Ngimwa ambaye aliteuliwa kuwa
Waziri wa Fedha na kupewa naibu wawili ambao nao hawakuwa katika duru za
kisiasa; Saada Mkuya Salum na Janeth Mbene. Ni wakati huohuo ambao
Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia aliteuliwa na Rais kuwa
mbunge.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment