Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
Na Mwandishi wa Thehabari.com
SERIKALI imetaja manufaa na faida ambazo wanatarajia
kuzipata wananchi wa Mtwara pamoja na Lindi endapo gesi itasafirishwa kwenda
Jijini Dar es Salaam.
Imesema Mkoa wa Mtwara ndipo utakapo jengwa mtambo mkubwa wa
kusafishia gesi hiyo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa
matumizi ya uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja viwandani.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, George Simbachawene alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45
kinachorushwa na Kituo cha Radio One jijini Dar es Salaam.
Naibu waziri huyo ameweka wazi kuwa mkoani Mtwara licha ya
Serikali kupanga kujenga viwanda vingine kadhaa, inajenga mtambo wa megawati
250 ambao utakuwa ukizalisha umeme na mwingine kujengwa mkoani Lindi eneo la
Somanga Funga utakao kuwa ukizalisha megawati 520.
Akifafanua zaidi Simbachawene alisema eneo la Mikindani
katika Kijiji cha Msijute mkoani Mtwara kinatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa
cha saruji Afrika Mashariki na Kati chenye uwezo wa kutoaji ajira kwa watu 6000
jambo ambalo ni manufaa ya Wanamtwara.
Alisema pia tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya mbolea
wamejitokeza kujenga viwanda mkoani Mtwara na Serikali itaviacha vinu vya
kuchimba na kusindika gesi eneo hilo
jambo ambalo bado ni manufaa makubwa kwa wananchi.
“Viwanda vya kusindika gesi hii vimepangwa kujengwa maeneo
ya Lubasi, Kishere, Mchinga Bay, Lindi, Sudi
Bay, Airport pamoja na
Mikindani…viwanda vyote hivi vitatoa ajira kubwa sana,” alisema Naibu Waziri.
Alisema licha ya manufaa hayo, gesi itakapopelekwa Dar es Salaam itazalisha
umeme wa uhakika pamoja na kutumika moja kwa moja viwandani jambo ambalo litailetea
taifa tija kubwa ikiwa ni pamoja kupunguza ukali wa maisha.
“Ni kweli gesi imepatikana Mtwara lakini ni lazima uipeleke
sokoni ili iweze kupata soko (wateja)…Dar es Salaam ndio kwenye soko, huwezi
ukaiacha Mtwara ambako hakuna soko; mbali na kuzalisha umeme kuna viwanda 37 na
hoteli kadhaa zinataka ziitumie moja kwa moja ni lazima iletwe huku, Mtwara
pale hakuna soko,” alisema.
Aidha alitolea mfano kuwa zipo nchi mbalimbali ambazo
zimegundua gesi lakini zimelazimika kuisafirisha kwa mabomba kwenda eneo la
soko. Alibainisha kuwa nchi ya Urusi inasafirisha gesi yake hadi nchini
Ujerumani huku Iran
ikisafirisha hadi India
gesi yake kutafuta soko lilipo.
Alisema miundombinu mikubwa ya umeme ipo jijini Dar es
Salaam hivyo kuna kila sababu ya gesi hiyo kuletwa jijini humo ili iweze
kuzalisha umeme na matumizi ya viwandani moja kwa moja pamoja na matumizi
mengine, ambapo tayari wateja wamepatikana.
Aidha aliongeza kuwa uzalishaji umeme wa kutosha kwa kutumia
gesi utapunguza bei ya umeme na kuuzwa kati ya senti 6 na 8 za Marekani jambo
ambalo litapunguza ugumu wa maisha na pia bei ya bidhaa nchini.
Pamoja na hayo amevitaka baadhi ya vyama vya siasa na
taasisi zisizo za Serikali (NGO’s) zinazowapotosha Wanamtwara juu ya mradi huo kuacha
kitendo hicho kwani hakuna asiyejua umuhimu wa gesi hiyo kuja Dar es Salaam.
“Hivi ni nani asiyejua kuwa tatizo la kutokua na umeme wa
uhakika nchini ndilo linalokwamisha uchumi wa nchi…Tanzania inapoteza bilioni 4.5 kwa
ajili ya kununua mafuta ya kuzalisha umeme kwenye mitambo yake, sasa gesi
itaokoa fedha hizi,” alisema Simbachawene.
Hata hivyo amesema Serikali haiwezi utekeleza mradi huo kwa
nguvu bali itaendelea kuwaelimisha Wanamtwara umuhimu na manufaa ya gesi hiyo
kuletwa Dar es Salaam na inaimani wataelewa na malumbano kumalizika.
*Imeandaliwa na
www.thehabari.com
You might also like:
No comments:
Post a Comment