Hatua hiyo imemshitua Rais Jakaya Kikwete ambaye amesema idadi hiyo
inaweza kuwa mzigo mkubwa kwa Taifa, jamii na uchumi wa nchi katika
kuwahudumia na kukidhi mahitaji yao ya msingi.
"Lazima tuwe na mipango madhubuti ya kiuchumi ili idadi hii ya watu
iweze kuhudumiwa," alisema Rais Kikwete na kuongeza: "Idadi hii ni kubwa
na naomba familia zingatieni uzazi wa mpango, vinginevyo hali ya maisha
itashuka kwani ushindani utakuwa mkubwa wa kupata huduma wakati
raslimali zilizopo ni ndogo na hazitoshelezi idadi hiyo."
Matokeo ya Sensa iliyofanyika Agosti 26 mwaka jana yanaonesha kuwa idadi
ya Watanzania kwa sasa ni milioni 44.9 na ifikapo mwaka 2016
itaongezeka hadi watu milioni 51.
Matokeo ya Sensa hiyo ambayo ni ya tano kufanyika nchini, yalitangazwa
jana na Rais Kikwete ambaye alionesha kushitushwa na kasi kubwa ya
ongezeko la watu nchini hadi akatoa mwito kwa Watanzania kuzingatia
uzazi wa mpango.
Katika takwimu hizo ambazo zinaonesha kuwa jumla ya Watanzania ni
44,929,002 kati yao idadi ya watu Tanzania Bara ni 43,629.434 na
Zanzibar idadi yao ni 1,303,568.
Mwaka 1967 ambako sensa ya kwanza ilifanyika wakati Tanzania ikiwa
Jamhuri ya Muungano, Watanzania walikuwa 12,313,054 kati yao Bara
walikuwa 11,958,954 na Zanzibar 354,400.
Sensa ya mwaka huu ilifanyika baada ya miaka 45 ya sensa ya kwanza
kufanyika na ongezeko la Watanzania kwa kipindi hicho ni watu milioni
33.
Kutokana na takwimu hizo, kasi ya ongezeko la watu kwa sasa ni asilimia
2.6 ikilinganishwa na takwimu za sensa ya mwaka 2002 ambayo ilionesha
kasi ya ongezeko la watu ilikuwa ni asilimia 2.9.
Sensa hiyo ilifanyika baada ya ile ya mwaka 2002 ambayo ilionesha kuwa
wakati huo Watanzania walikuwa milioni 34.4, hivyo ndani ya miaka 10
Watanzania ambao wameongezeka ni milioni 10.5.
Rais Kikwete alisema idadi hiyo kwa mtazamo wa haraka haraka na kwa
ukubwa wa nchi, inaweza kuonekana kuwa ndogo, lakini akaonya kuwa uwezo
wa nchi kiuchumi ndio unafanya idadi hiyo ionekane kubwa.
"Idadi ya watu ni kubwa, maana yake ni kwamba Serikali tujipange vizuri
kwa ongezeko hili kubwa na tutafanya sehemu yetu, lakini jamii nayo
ifahamu kuwa ushindani wa kupata huduma utakuwa mkubwa hivyo nao
wazingatie uzazi wa mpango," alisema Rais Kikwete.
Matokeo yaliyotangazwa jana kwa mujibu wa Rais Kikwete ni ya awali na
ifikapo Februari takwimu za kujua idadi ya wanawake na wanaume
zitatolewa na Aprili takwimu za kujua rika la watu kila wilaya
zitatolewa na za mwisho zitatolewa Juni 2014.
Katika matokeo hayo mengine, pia itajulikana idadi ya wazee waliopo,
vijana na nguvukazi inayofanya kazi sasa. Takwimu hizo kwa mujibu wa
Rais Kikwete zitatumiwa na wadau wengine kama nchi wahisani na asasi
zisizo za serikali.
Rais alisema sensa italigharimu Taifa Sh bilioni 140 ambapo kwa sasa
tayari Sh bilioni 124 zimetumika. "Sensa inafanywa na kila Taifa duniani
kote na ni gharama kubwa kuhesabu watu."
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu
Mizengo Pinda alisema sensa hiyo imegharimiwa kwa pamoja kati ya
Serikali na washirika wa maendeleo. Alisema mchango wa Serikali katika
kugharimia sensa umekuwa ukiongezeka kutoka sensa moja hadi nyingine.
Alisema sensa ya mwaka huu, Serikali imechangia asilimia 90 ya gharama
zote kutoka asilimia 70 kwa sensa ya mwaka 2002. Alisema sensa hiyo pia
kwa kiasi kikubwa imeendeshwa na wataalamu wa ndani kuliko ilivyokuwa
kwa sensa iliyopita.
"Hii inaonesha kukua kwa wataalamu wa ndani katika uendeshaji wa sensa
na utafiti mwingine hapa nchini," alisema Pinda na kufafanua kuwa
utekelezaji wa kuhesabu watu ulitoa ajira ya muda mfupi kwa wananchi
hususan vijana ambao hawakuwa na ajira.
Alitaja idadi ya watu 150 kuwa walipata ajira ya kutenga maeneo ya
kuhesabia watu ambapo makarani na wasimamizi wa sensa walikuwa 200,000
wakati wachambuzi wa takwimu walikuwa 400 walioajiriwa kwa vipindi
tofauti wakati wa kutekeleza sensa. Wazabuni wa ndani wapatao 29 walitoa
huduma na vifaa mbalimbali kwa ajili ya la sensa kwa Sh bilioni 11.7.
Changamoto kadhaa zilizojitokeza zilitajwa na Pinda kuwa ni pamoja na
watu wanne kupoteza maisha walipokuwa wakiwajibika na kazi hiyo na
wengine kadhaa kujeruhiwa.
Rais Kikwete alitaja pia changamoto zingine kuwa ni watendaji wa sensa
kukumbana na purukushani kutokana na kundi la watu waliotishia kuvuruga
sensa na wengine kufanya kampeni ya kushawishi watu wasusie kuhesabiwa.
"Wengine katika kipindi hiki ndicho walipanga kufanya maandamano na
mikutano, lakini pamoja na changamoto zote hizi, tumefanikiwa," alisema
Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment