ASEMA SPIKA, MAWAZIRI WASIWE WABUNGE
SPIKA wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, amependekeza
kuwa katika Katiba Mpya ijayo iruhusu kuwapo kwa mabunge mawili; yaani
hili la sasa na jingine la seneti kama ilivyo kwa nchi za Marekani na
Uingereza.
Makinda
alisema kuwa sababu kubwa ya kuwapo kwa mabunge hayo ni kutokana na
viwango vya elimu vya wabunge wengi wa sasa kuwa vya kawaida, hivyo
kuhitaji Bunge la seneti litakalokuwa na wabunge wenye upeo zaidi.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha maoni yake kwenye Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Makinda alisema wabunge wa sasa wamekuwa na
tabia ya kujadili hoja za kitaifa lakini mwishowe wanazigeuza kuwa za
vyama vyao.
“Kuna
umuhimu wa kuwa na Bunge la seneti ambalo wabunge wake watakuwa na
uzoefu wa kutambua na kupambanua mambo kwa masilahi ya taifa bila
kuingiza vyama,” alisema.
Makinda pia
alisema kuwa katiba mpya itamke kuwa Spika wa Bunge asitokane na vyama
vya siasa na asiwe mbunge ili awe na maamuzi huru badala ya kutetea
vyama.
Pia alisema
kuwa, kwa sababu shughuli za Bunge zimekuwa nyingi na Bunge limepanuka,
amependekeza wawepo manaibu katibu wawili watakaosaidiana kuendesha
shughuli za Bunge.
Aliongeza
kuwa amependekeza mawaziri wasiwe wabunge ili wafanye kazi kwa usawa,
kwani kwa sasa usawa haupo kutokana na mawaziri wengi kupendelea majimbo
yao.
Aidha,
alisema kuwa viti maalumu vinahitajika kuwapo, kwani mfumo dume bado upo
majimboni, na kueleza kuwa vikiondolewa wanawake watakuwa nyuma, lakini
akaongeza kuwa kwa sasa wanawake bado wanaendelea kuelimika.
Kuhusiana na
kuweka ukomo wa ubunge, alisema kuwa hakuna sababu, kwani kuna baadhi
ya wabunge wanang’ara majimboni kwao kutokana na kutimiza ahadi zao kwa
wananchi.
Naye Jaji
Mkuu, Chande Othman Chande, alisema kuwa amependekeza katiba mpya ilinde
kwa namna yoyote Mahakama, kwani si mhimili unaofungamana na upande
wowote, hivyo usiingiliwe na siasa, kwani ni sehemu pekee haki
inapopatikana.
Alisema kuwa
wamependekeza katiba mpya itambue haki ya mwananchi kupata fursa ya
kupata haki na Serikali iwajibike kumpa mwananchi fursa ya kupata haki,
kwani kwa sasa Tanzania haimpi mwananchi haki.
“Nipo hapa
kutoa maoni kwa niaba ya watenda kazi wote wa Mahakama, majaji, mahakimu
na wafanyakazi wengine wapatao 6,000, lakini sisi tunataka katiba mpya
impatie mwananchi haki ya kupata fursa ya kupata haki, kwa mfano kuna
mikoa 12 haina mahakama kuu na wilaya zaidi ya 25 hazina mahakama za
wilaya, sasa katiba itoe fursa ya kupata haki yake,” alisema.
Pia alisema
kuwa katiba mpya itambue nchi inatawaliwa na misingi ya katiba, pia
utawala wa sheria utawale lakini katiba ya sasa haisemi hivyo, ikiwemo
mihimili yote kuongozwa na katiba.
Kuhusu
uteuzi wa majaji, alisema kuwa wamependekeza katiba mpya ipanue Tume ya
Utumishi wa Mahakama, kwa kutoka majaji sita wanaounda tume hiyo na
kufikia 12.
Alisema kuwa
wanapendekeza watakaoongezwa wawe ni mtumishi wa Mahakama, mtu wa
kawaida, haki za binadamu, tume ya umma, mawakili na mkufunzi wa Kitivo
cha Sheria ili rais ashauriane na tume hiyo katika kuteua majaji.
No comments:
Post a Comment