MBUNGE wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Mikindani, Ali Chinkawene wamepinga kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba wakazi wa Mkoa wa Mtwara hawapaswi kuzuia gesi kwenda Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuunga mkono
wakazi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam.
Kulia ni Katibu wa Kampeni na Uchaguzi NCCR, Faustine Sungura. Picha na
Michael Jamson
Juzi, katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Kikwete alipinga madai ya
wakazi wa Mikoa ya Kusini kutaka gesi hiyo isisafirishwe kwenda Dar es
Salaam, akisema madai hayo hayakubaliki popote.
“Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii ni mali ya taifa zima
na hutumika kwa manufaa ya taifa na katu si mali ya watu wa pale
ilipogundulika au pale shughuli inapofanyika,” alisema Rais Kikwete.
Viongozi hao mbali na kuonyesha misimamo ya kuzuia nishati hiyo hata
kabla ya kauli hiyo ya Rais Kikwete, jana walisisitiza kwa nyakati
tofauti kwamba, wataendelea kuunga mkono jitihada za wananchi kupinga
usafirishwaji wake kwa kuwa hiyo ni haki yao.
Murji alisema yupo tayari kuvuliwa ubunge kwa kutetea masilahi ya
Wanamtwara wanaopinga gesi hiyo inayovunwa katika Kijiji cha Msimbati,
mkoani Mtwara huku Chinkawene akisema msimamo wa chama chake ni kuungana
na wananchi kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Alisema Serikali inapaswa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme mkoani
Mtwara badala ya Dar es Salaam... “Tulipoona hali inakuwa tete,
niliitisha kikao cha Kamati ya Siasa kujadili nini msimamo wa chama
katika hili. Kamati ya Siasa wakasema hawawezi kukisemea chama kwa
sababu chama ni wanachama, hivyo nikaitisha kikao cha Halmashauri Kuu
ambapo pia tuliwaalika mabalozi wa mitaa.”
“Katika kikao hicho, wajumbe walipinga kwa nguvu zote suala la gesi
kupelekwa Dar es Salaam. Wakaniambia niseme msimamo wao kuwa hawataki
gesi iende Dar es Salaam hadi pale masilahi ya Wanamtwara yatakapowekwa
wazi na Serikali.”
Mwenyekiti huyo alisema kwa maana hiyo, msimamo huo si wake binafsi,
bali ni maazimio ya vikao halali vya chama hicho vinavyowakilisha
wanachama na kwamba historia ya Mikoa ya Kusini jinsi ilivyonyimwa
maendeleo ilitumiwa na wajumbe kujenga hoja hiyo.
“Wakati sisi hatuna umeme hakuna aliyefirikia kutuunganisha kwenye gridi
ya Taifa… Barabara ya kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam miaka 51 ya
Uhuru sasa, haijakamilika. Lakini bomba wanataka kujenga kwa miezi 18.
Hivi kuna Watanzania muhimu zaidi ya wengine?” alihoji Chinkawene
akinukuu kauli za wajumbe wa kikao hicho na kuongeza:
“Walizungumza mambo mengi, suala la kung’olewa kwa reli, kukatazwa
kulima pamba, kuuawa kwa kilimo cha karanga na mkonge. Haya yote wanadai
yamesababisha mkoa uendelee kuwa maskini na kwamba tumaini lao limebaki
kwenye gesi. Wamesema wapo pamoja na wananchi.”
Murji kwa upande wake, alisema amekutana na umoja wa vyama vya siasa
vilivyoratibu maandamano ya kupinga suala hilo na kuwapongeza kwa kazi
nzuri akisema wananchi wana haki ya kutetea rasilimali yao.
Alisema yeye si mbunge anayewakilisha mawazo yake bungeni, bali ya
wananchi... “Hivyo ni bora niungane na wananchi wangu kutetea masilahi
yao; liwalo na liwe.”
“Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa kwa ujasiri na uthubutu wenu wa
kutetea rasilimali hii (gesi)… Tusidharau hata kidogo malalamiko ya
wananchi…” alisema Murji huku akishangiliwa na wajumbe na kuongeza:
“Nipo pamoja nanyi na hata ikibidi nivue ubunge, nipo tayari kufanya hivyo kwa masilahi ya wananchi….”
Chanzo: Mwanachi
No comments:
Post a Comment