ASEMA KAULI ZA WAZIRI MUHONGO NI HATARI
NAIBU Katibu Mkuu wa Chadena, Kabwe Zitto, na wenyeviti wa vyama vya
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi,
wameishukia serikali wakisema inaweweseka kutokana na kauli ya Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kukinzana na mkakati wa
serikali.
Hatua hiyo inakuja siku moja tangu Waziri Muhongo akutane na waandishi
na kuwakejeli wananchi wa mikoa ya kusini hususan Mtwara kuwa
hawakupaswa kuandamana kupinga mpango wa serikali kusafirisha gesi
kutoka huko kwenda Dar es Salaam kwa kuwa rasilimali ni za Watanzania
wote.
Waziri Muhongo alidai kuwa wananchi wa Mtwara wanashawishiwa na
wanasiasa ili kufanya vurugu ilhali gesi nyingi haiko kwao bali iko
kwenye mipaka ya nchi baharini kwenye kina kirefu na kuongeza kuwa hata
wao wamekuwa wakinufaika na rasilimali za mikoa mengine.
Katika taarifa yake, Zitto alisema kuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara aliwaita
Watanzania wa mkoa huo wahaini, wapuuzi na watu hatari huku Rais wa
Jakaya Kikwete naye akiingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu
wanaowaunga mkono wawanachi hao akiwaita watafuta umaarufu wa kisiasa na
wanataka kuigawa nchi.
“Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri Muhongo alifanya mkutano na
waandishi wa habari kueleza suala lilelile ambalo bosi wake alilielezea
usiku wa kuamkia Mwaka Mpya 2013. Hii ni dalili ya serikali kuweweseka,”
alisema.
Alisema kuwa katika kauli ya serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya
wimbo uleule wa ‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ serikali ilitaka
kuonyesha umma kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani.
Kwamba miaka yote toka Uhuru watu wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na
pamba, kahawa, chai, tumbaku na sukari na hivyo watu wa Mtwara na Lindi
hawakuchangia hata kidogo kwenye hazina ya taifa.
“Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa
shukurani. Kauli ya serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa
uhalali wa kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata tamaa. Ni kauli hatari
sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yao.”
Zitto alifafanua kuwa serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba
toka Uhuru watu wa Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana
katika uchumi wa taifa kupitia zao la korosho.
Alisema takwimu za uzalishaji wa korosho zinaonyesha kwamba kuanzia
mwaka 1965 mpaka 2011 zimeliingizia taifa fedha za kigeni jumla ya dola
za Kimarekani bilioni 4.58. Katika mwaka wa uchumi unaoishia Novemba
2012, korosho imeliingizia taifa jumla ya dola za Kimarekani 151
milioni. Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza dola milioni 130 wakati
pamba iliingiza dola 53 milioni tu.
Zitto alihoji kuwa tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi asilia kuzalisha
umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio inaifanya
serikali kusahau kabisa kujitoa muhanga kwa watu wa Mtwara katika
kulinda uhuru wa taifa letu?
Kwamba serikali kusema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu ndiyo
inazalisha asilimia 80 ya mapato ya serikali ni uongo na aibu serikali
kujitetea kwa uongo.
“Dar es Salaam ni kituo tu cha kukusanyia mapato ya serikali. Uzalishaji
mkubwa wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es
Salaam. Walipa kodi wakubwa wengi ofisi zao kuu ziko Dar es Salaam
lakini uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es Salaam.
Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji halisi
wa mapato hayo unafanyika wapi,” alihoji. Zitto alisistiza kuwa
maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya
Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za serikali.
Alisema kuwa watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la
Songosongo. Hata kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (asilimia 0.3)
ilikuwa inalipwa na Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan
Africa Energy.
Lipumba, Mbatia wanena
Akizungumza na gazeti hili, Profesa Lipumba alisema anashindwa kumwelewa
Waziri Muhongo, hajui hali halisi ya maeneo ya Watanzania, kama hawezi
kusema gesi iko maeneo gani katika mikoa ya Tanzania, basi ni profesa wa
ajabu kidogo.
Alifafanua kuwa anashindwa kumwelewa kwani anapingana na sera ya serikali ambayo yeye mwenyewe ni waziri.
Alisema kuwa kama gesi ilipoanza kuchimbwa Songosongo likajengwa bomba
dogo la nchi 12 kusafirisha gesi chini ya bahari toka Songosongo hadi
Somanga na bomba la nchi 14 lilijengwa toka Somanga hadi Dar es Salaam.
“Uwezo wa mabomba haya ni mdogo ukilinganisha na gesi inayopatikana
Songosongo na mahitaji yake kwa shughuli ya kufua umeme na kutumia
viwandani,” alisema.
Alisema kuwa mpango huu ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika
Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme, kwamba mradi huo wa
kufua umeme MW 300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka huu wa 2012.
Lipumba aliongeza kuwa wananchi wa Mtwara wanahitaji kujua kwa nini
serikali haikutafuta njia mbadala ya kugharamia mpango wa kufua umeme na
kuiunganisha Mtwara na gridi ya taifa.
Naye Mbatia akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa anashangazwa
na viongozi wa CCM wanaposhindwa kuwa na sauti moja ya kusimamia
rasilimali za taifa na hivyo kuparaganyika na kupishana kauli katika
suala la gesi.
“Hatuhitaji viongozi wa kuuliza Watanzania tunataka nini, Watanzania
wote tunataka kushirikishwa hasa katika masuala ya rasilimali ya gesi,
maumivu ya mikataba mibovu katika sekta ya madini na sekta nyingine
imetuchosha,”alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Helen
Kijo-bisimba, pamoja na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, Ussu
Mallya, walisema wananchi hawana tatizo isipokuwa serikali
haijawashirikisha kwani wanajua kuwa mikoa yao imeachwa nyuma muda mrefu
bila maendeleo.
No comments:
Post a Comment