MBUNGE wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo ametangaza kuchukua kile alichokiita uamuzi mgumu ili kuhakikisha kuwa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa anamrithi Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Shelukindo alitoa kauli hiyo Jumapili wakati
akiwasalimia wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa
Hosteli ya KKKT katika sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika
nyumbani kwa Lowassa ambazo pia zilihudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.
Jana alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Shelukindo
alisema: “Ni kweli mimi ni muumini wa Lowassa, ila pale (mkutanoni)
sikumtaja kwa sababu najua chama kina taratibu zake na muda wa mchakato
wa kumpata Rais haujafika.”
“Niliposimama niliwaeleza kuwa nisingeweza
kuchangia fedha nyingi kwa sababu watu wangu wana njaa huko Kilindi. Pia
kule (Kilindi) tunaendesha harambee ya aina hiyohiyo. Ila nikawaambia
zawadi yangu kwa Wanamonduli ni kufanya uamuzi mgumu ili mwaka 2015
apatikane Rais mzalendo na anayeweza kufanya uamuzi mgumu na kwa
wakati.”
Shelukindo aliendelea: “Niliposema hivyo, umati
uliibuka kwa shangwe na kunitaka nimtaje nitakayeshirikiana naye, lakini
nikawaambia kuwa huu si wakati mwafaka ila baadaye nilichangia
Sh500,000.”
Shelukindo alisema harambee hiyo ilitarajiwa kuchangishwa Sh100 milioni lakini zikapatikana Sh70 milioni.
Mbali na Shelukindo, makada wengine wa CCM
waliohudhuria sherehe hizo ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew
Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mngeja.
Awali, akizungumza katika sherehe hizo, Lowassa
aliwataka Watanzania kutumia mwaka huu wa 2013 kufanya uamuzi mgumu
katika kila changamoto inayowakabili.
“Salamu zangu za Mwaka Mpya kwa Watanzania:
Nawaomba wapitishe uamuzi mgumu kwa kila changamoto watakazokabiliana
nazo,” alisema. Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na
umaskini na kuongeza kuwa mtu akiamua inawezekana.
Lowassa aliwahi kusema bungeni akiitaka Serikali
kuwa na tabia ya kupitisha ‘uamuzi mgumu’ katika kuwaondolea wananchi
kero akisema bila kuthubutu ni vigumu kukabiliana na changamoto.
Katika sherehe hizo, Lowassa pia alizungumzia
taarifa zilizozagaa mitandaoni kuwa sherehe yake hiyo ilikuwa ni ya
kisiasa akisema: “Wameandika katika mitandao ya kijamii kuwa kuna
sherehe kubwa ya kisiasa. Mimi nawaambia wa waache porojo hizo. Nimekuwa
nikiandaa sherehe hizi tangu mwaka 1995, wao wakitaka waige mfano huu.”
Mwananchi.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment