MBUNGE wa Jimbo la Iringa ,Mchungaji Peter Msigwa amewataka wakazi wa
Kijiji cha Kigonzile, katika Manispaa ya Iringa kutomchagua katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ikiwa hatatimiza ahadi ya kuwapelekea maji
na barabara katika kipindi hiki cha uongozi wake.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule
ya Msingi Kigonzile juzi, Msigwa alisema amepania kuwafikishia maji na
barabara wakazi wa kijiji hicho ili kuwapunguzia kero ya kutafuta maji
na adha ya usafiri.
“Ninajua kero ya maji na barabara ndizo zinazowatesa wakazi wa kijiji
hiki hususani wakina mama, lakini niseme tu kwamba suala la maji,
nimefurahi kuna mfuko mnaendelea kuuchangia deni lililobaki
ninalimalizia sasa na kuhusu barabara tayari nimeshaleta greda
nitahakikisha barabara hii inatengenezwa, nisipotimiza ahadi hizi
msinipigie kura mwaka 2015,”alisema Msigwa.
Aliwataka wamhukumu kwa ahadi zake kwani atayafanya hayo katika kipindi cha miaka miwili.
Katika mkutano huo, Msigwa alitoa Sh1.06 milioni kwa ajili ya ujenzi wa
mradi wa maji unaotekelezwa kwa ubia na wananchi pamoja na Serikali kwa
msaada kutoka Benki ya Dunia.
Katika mradi huo wananchi walitakiwa kuchanga Sh3 milioni ambapo hadi
mbunge anakwenda kufanya mkutano juzi walikuwa wamechanga Sh1.04 milioni
.
Mwenyekiti wa kamati ya maji wa kijiji hicho, Emsy Silla alisema fedha
zilitakiwa kuchangiwa na wananchi ni Sh3 milioni ambapo zingechanganywa
na michango mingine kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Manispaa kwa
ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Katika mkutano huo wakazi wa kijiji hicho walilalamikia kukosekana kwa huduma mbalimbali za kijamii katika kijiji chao ikiwamo huduma za afya na maji safi na salama wakidai hali hiyo inahatarisha maisha yao.
Katika mkutano huo wakazi wa kijiji hicho walilalamikia kukosekana kwa huduma mbalimbali za kijamii katika kijiji chao ikiwamo huduma za afya na maji safi na salama wakidai hali hiyo inahatarisha maisha yao.
Akijibu hoja hizo mbunge huyo alisema suala la kukosekana kwa huduma ni
tatizo la kitaifa na kwamba limekuwa likilalamikiwa katika maeneo yote
nchini lakini akasisitiza uchache wa idadi ya wabunge wa chama chake
unachangia kupitishwa bajeti isiyokidhi huduma za afya.
Chanzo: mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment