Pages


Photobucket

Saturday, June 1, 2013

SIRI YA KUTEKWA ABSALOM KIBANDA YAANIKWA, ISOME HAPA

Timu ya kuchunguza tukio la kutekwa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda (pichani), imebaini kuwa kazi yake ya uandishi wa habari na siasa vimechangia kuvamiwa kwake na kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Aidha, uchunguzi wa timu hiyo umebainisha kuwa baadhi ya watu waliohojiwa walidai kuwa utekaji wa Kibanda ulifanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivyo kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vitendo vya ugaidi. 
Taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa timu hiyo, Deodatus Balile, iliyoundwa na TEF katika mkutano wa pili wa mwaka wa mashauriano kati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na jukwaa hilo jijini Tanga.
“Uchambuzi uliofanywa na timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:- Kazi yake ya uandishi wa habari, Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali, uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi na vitendo vya rushwa,” ilieleza taarifa hiyo.
Alisema timu hiyo imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hilo kwani waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba kushambuliwa na kuumizwa Kibanda halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.
Imeeleza kuwa kazi yake ya uandishi wa habari na siasa vikiunganishwa vimechangia kuvamiwa kwa Kibanda na kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa waliohojiwa waliyataja matukio ya uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro ya  Chadema na mkanda anaodaiwa kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, kuwa vililenga kukifanya chama hicho kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kuwaumiza.
“Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga kukifanya Chadema kionekane cha kigaidi mbele ya macho ya jamii, ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia kujenga hoja hiyo,” taarifa hiyo ilieleza.
Aidha, baadhi ya watu waliohojiwa walidai kuwa Chadema kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa, hivyo wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.
Imeeleza kuwa kwa njia hiyo, hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani na kauli ya Chadema kuwa nchi haitatawalika itakuwa imetimia.
Taarifa zaidi ya kamati hiyo imebainisha kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini kutokana na makundi mengi yenye maslahi kuwaona wanahabari wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa maslahi yao haramu. 
“Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015,” taarifa hiyo ilisema.
Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari tofauti na zamani wakati ambao habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la Mwandishi wetu, lakini siku hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani ameandika habari fulani.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. 
Taarifa hiyo inamnukuu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Dk. Reginald Mengi akisema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi wataumia.”
Taarifa ya kamati hiyo inabainisha kuwa mazingira ya kazi ndani ya Kampuni za New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu na ndani ya New Habari kumekuwapo na misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia ya habari kwa ujumla.
“Mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si mzuri. 
Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda, uchunguzi huo umebainisha. 
Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.
“Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe, alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda.” 
Kibanda alitekwa usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, mwaka huu  na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake  eneo la Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, Kibanda aliumizwa kwa kutobolewa  jicho la kushoto, akaumizwa kichwani kiasi cha kusababisha  kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. 
Aidha watekaji walimng’oa meno mawili na kucha mbili, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.
Wakati timu hiyo iliyowashirikisha Balile, Pili Mtambalike , Jane Mihanji, Tumaini Mwailenge na Rashid Kejo ikiwasilisha taarifa yake, timu iliyoindwa na jeshi la Polisi kuchunguza tukio hilo hadi sasa haijafanya hivyo, badala yake imekuwa ikisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea.
 
habari NA THOBIAS MWANAKATWE
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment