Pages


Photobucket

Monday, June 24, 2013

PEP GUARDIOLA ANAWEZA ASIDUMU BAYERN MUNICH - MATTHIAS SAMMER TATIZO.



Kocha aliyeipa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya klabu ya Bayern Munich, Jupp Heynckes ameshaachia ngazi katika nafasi yake na sasa Pep Guardiola aliyekuwa akiinoa Barcelona ndiye aliyechukua mikoba yake.

Hii ni habari nzuri kwa mashabiki wa Bayern, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba furaha ya mashabiki hao itakuwa ya muda mfupi kwani Guardiola naye atatimuliwa au kuondoka ndani ya muda mfupi ujao kutokana na asili ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Heynckes anaweza kuonekana kocha bora aliyeiongoza Bayern kutwaa mataji matatu ndani ya msimu mmoja lakini nyuma ya pazia kuna siri moja kubwa iliyokuwa imejificha, ambayo hata Guardiola atakumbana nayo atake au asitake. 

Nyuma ya mafanikio yote ya Bayern msimu huu ya kutwaa taji la Ulaya, Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’ na Kombe la Ujerumani, kuna mtu anayeitwa Mathias Sammer, huyu ni beki wa zamani wa klabu ya Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani.

Sammer ndiye mkurugenzi wa ufundi wa Bayern ambaye pia ana taaluma ya ukocha, huyu ndiye kila kitu ndani ya timu hiyo kwa sasa na kuna habari kwamba hata kikosi cha timu hiyo hukipanga yeye, tena kwa maelekezo mengine muhimu kwa kocha.

Kama inakumbukwa, Sammer ni mshindi Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka 1996 akiiwakilisha Ujerumani iliyokuwa na wakongwe kadhaa akiwemo mshambuliaji hatari, Jurgen Klinsmann.

Matthias Sammer

Pia Sammer amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1996 akiiwakilisha Dortmund ambayo mwaka huu aliifunga katika fainali ya michuano kama hivyo. Huyu ndiye Sammer.

Mtindo huu wa Sammer na maafisa wenzake wa Bayern kuwapangia makocha vikosi ili kupata uhakika wa ushindi unatabiriwa kuendelea hata kwa Guardiola ambaye kwa tabia zake ni wazi atakataa hali hiyo na kutimka zake.

Heynckes anaondoka Bayern kwa mambo mengi ikiwemo kuelezwa kwamba ana uwezo mdogo lakini ukweli ni kwamba, haridhishwi na tabia ya Sammer na watu wake ya kumpangia kikosi tena kwa ulazima bila ya...... kufuatwa kwa ushauri wake.

Makocha wengi wa Ulaya hupata wakati mgumu wanapokuwa chini ya wakurugenzi wa ufundi ambao wamewahi kucheza soka kwa mafanikio, kwani hujifanya wajuaji na kuweza kupanga au kuamua jambo lolote na wakati wowote.

Tazama leo hii jinsi maafisa wa Newcastle United wanavyomtazama kwa jicho baya Joe Kinnear ambaye ni mkurugenzi mpya wa ufundi, tayari Kocha Alan Pardew ameshapiga mkwara wa kutoingiliwa katika maamuzi yake kama kocha.

Kinnear aliifundisha Newcastle katika msimu wa 2008/09, hivyo anajua kila kitu cha uwanjani na hawezi kuacha akiona timu inazama bila ya kutoa maagizo au kuamuru kocha kufanya jambo fulani.

Makocha hawapendi kuingiliwa katika maamuzi labda mikataba yao iweke wazi kuhusu hilo. Kwa Afrika hii ni hali ya kawaida lakini Ulaya na sehemu nyinginezo ambazo soka limepiga hatua, makocha huamua kujiuzulu.

No comments:

Post a Comment