Pages


Photobucket

Wednesday, June 26, 2013

Meli ya Magufuli yazama, wajanja wamekuwa wakiingia na kukata vyuma vya meli hiyo


ILE meli maarufu kwa jina la ‘Meli ya Magufuli’ ambayo serikali iliinasa katika eneo lake la bahari ya Hindi ikivua samaki bila ya kibali, imezama baharini, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
 Meli hiyo ambayo ina uwezo wa kuvua samaki kwenye kina kirefu baharini, imezama  baada ya wajanja wachache kukata vyuma vyake na kuuza kama chuma chakavu.
Kwa mujibu wa habari hizo, wajanja wamekuwa wakiingia na kukata vyuma vya meli hiyo baada ya serikali kuitelekeza kwa muda mrefu bila uangalizi tangu ilipoitaifisha.
Vyanzo vya habari vilipasha kuwa vyuma chakavu vya meli hiyo vimekuwa vikiuzwa kwa kampuni zinazonunua na kuvisafirisha nje ya nchi na kujiingizia mabilioni ya fedha.
Sehemu kubwa ya vyuma chakavu kutoka kwenye meli hiyo, vimeuzwa kwa kampuni moja inayomilikiwa na mmoja wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano.
Inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya meli hiyo imetengenezwa kwa malighafi aina ya Brass ambayo kilo moja kwa sasa inauzwa kwa sh 5,200.
Malighafi nyingine zilizotumika na bei yake kwa kilo kwenye mabano vikuzwa kama chuma chakavu ni Cast Aluminum (sh 1,700), Stainless (sh 1,500) na Soft (sh 2,000).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia meli hiyo, alisema yuko mkutanoni na kutaka atafutwe baadaye kutolea ufafanuzi.

Akizungumza  kwa njia ya simu, Waziri Mathayo alikiri kuwa kweli meli hiyo imezama na amepata taarifa hizo.
“Ni kweli imezama na sisi tumepata taarifa hizo, lakini kama wizara tulikuwa hatujakabidhiwa meli hiyo kwani ilikuwa kielelezo cha polisi wakati kesi ilipokuwa mahakamani na haijawahi kukabidhiwa kwetu,” alisema Waziri Mathayo.
Meli hiyo, Tawaliq 1, ilikamatwa Machi 8, 2009 ikiwa na tani 293 za samaki aina ya Jodari iliyowavua katika bahari ya Hindi ndani ya Ukanda wa Kiuchumi wa Tanzania (EPZ) bila kibali.
Ilikamatwa ikiwa na wavuvi 34 na hadi kufikia tamati ya kesi hiyo, 20 walitiwa hatiani.
Lakini licha ya mahakama kuamuru meli hiyo itaifishwe kwa sababu ilikuwa haijulikani na tume inayojihusisha na shughuli za uvuvi katika Bahari ya India (IOCT) ilitelekezwa.
Kwa mujibu wa habari hizo, meli hiyo ilianza kuzama tangu mwaka jana huku wizara husika ikiangalia bila kuchukua hatua.
Meli hiyo ilikamatwa na Waziri Dk. John Magufuli mwaka 2009 wakati huo akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi

No comments:

Post a Comment