Pages


Photobucket

Friday, February 1, 2013

SAKATA LA GESI MTWARA: Mbowe ambana Pinda


Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mwenyekiti  wa
CHADEMA Freeman Mboe
KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amembana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitaka serikali iwachukulie hatua watendaji waliozembea kudhibiti vurugu za mzozo wa gesi Mtwara.

Mbowe pia alimhenyesha Pinda akimtaka alihakikishie Bunge ni lini serikali itakuwa tayari kuweka wazi mikataba kadhaa ikiwamo ya mafuta na gesi asili ili kuondoa upotoshaji wa miradi hiyo kama ilivyotokea Mtwara.
Akiuliza swali hilo bungeni jana mjini hapa, Mbowe alisema kwa kuwa vurugu hizo zimetokana na uzembe wa kisiasa na viongozi wakiwamo wa vyombo vya dola kushindwa kubaini na kudhibiti ghasia hizo mapema, kwanini wasichukuliwe hatua kwa uzembe huo.
Akijibu maswali hayo, Pinda alirejea kauli yake ya mara kwa mara tangu alipotoka kusuluhisha mzozo huo Mtwara, akisema vyama vya siasa vimechangia sana kukuza na kupotosha ukweli wa mradi huo.
Alisema wanasiasa walitumia mzozo huo kujiimarisha kisiasa na kujijenga kwa ajili ya uchaguzi unaokuja. "Suala la kuwawajibisha watendaji hao liko chini ya waziri mkuu na rais, tutaliangalia,” alisema Pinda.
Hata hivyo, Pinda alisema jambo la msingi si kutafuta mchawi, kwani tatizo la Mtwara ni la wote, na siku zijazo kutakuwa na ushirikishwaji wa jamii katika kutoa elimu ili kuepuka madhara kama yaliyotokea Mtwara.

Kuhusu kuweka wazi mikataba ili kuondoa upotoshaji, Pinda alisema mikataba hiyo haina siri na inaweza kuwekwa wazi kupitia mifumo ya kibunge.

Hata hivyo, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hakuridhika na majibu hayo na katika maswali yake ya nyongeza alimtaka waziri mkuu kutamka wazi bila kumng’unya maneno kama serikali iko tayari kuweka mikataba hiyo wazi.
Pia alihoji ni kwa nini serikali iko tayari kutekeleza kero za wananchi pale inapobanwa kwa presha na maandamano kama ilivyotokea Mtwara.
Katika hoja hiyo, Pinda alisema serikali haiko tayari kuweka wazi mikataba hiyo kupitia magazeti, kwani mingine ina taratibu zake lakini iko tayari kuweka wazi kupitia mifumo ya kibunge.
Kuhusu serikali kusikiliza kero za wananchi baada ya presha za maandamano, Pinda alisema maandamano si njia sahihi ya kuwasilisha madai ya wananchi.
"Ndugu yangu Mbowe anajaribu kuleta hoja ambayo haina mashiko. Mimi siamini kuwa maandamano ndiyo njia sahihi ya kuwasilisha malalamiko ya wananchi,” alisema Pinda.
Mapema kabla ya maswali kwake, Pinda alitoa taarifa ya kueleza kuhusu vurugu za Mtwara pamoja na madhara yaliyojitokeza, ambapo hata hivyo alirudia kile alichowaeleza waandishi wa habari juzi.
Alisema kulikuwa na upotoshaji mkubwa kwamba bomba hilo la gesi lingeishia Bagamoyo ambako inajengwa bandari ya kusafirishia gesi hiyo nje na kumhusisha Rais Jakaya Kikwete, jambo ambalo si la kweli kabisa.
Waziri Mkuu Pinda aliwatangazia wabunge uharibifu wa mali na hasara iliyopatikana kutokana na vurugu hizo, sambamba na kuorodhesha majina ya watu waliochomewa nyumba, magari na mali nyingine.
Pia alitaja majengo na ofisi za serikali zilizochomwa moto pamoja na magari, ambapo uharibifu huo umesababisha hasara ya mabilioni ya fedha, akisema serikali itaangalia namna ya kuwafidia.
Mbunge amwaga machozi
Wakati akitaja majina ya watu waliochomewa nyumba na mali zao, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kasembe, alitokwa machozi ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Hali hiyo ilifanya baadhi ya wabunge wanaokaa jirani naye kumtoa nje ya ukumbi na kumbembeleza huku wakimpa pole.
Mbunge huyo ni mmoja wa wabunge waliochomewa nyumba, magari na mali nyingine.
Wengine ni Anna Abdallah na Hawa Ghasia, ambao nyumba zao ziliteketezwa kabisa.
Tume ya Spika yayeyuka
Spika wa Bunge, Anne Makinda, ametengua uamuzi wake wa kutaka kuunda kamati ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza sakata la vurugu za Mtwara.
Akitangaza uamuzi huo jana, Makinda alisema baada ya taarifa ya waziri mkuu kuhusu mzozo huo, hakuna haja ya kuunda tume hiyo.
"Kwa vile taarifa ya serikali imejitosheleza, Bunge hatuna sababu tena ya kuunda tume. Nampongeza waziri mkuu kwa kazi aliyoifanya na niwapongeze wananchi wa Mtwara kwa kuelewa na kudumisha amani,” alisema.
Mnyika awapinga
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema hajaridhika na taarifa ya waziri mkuu pamoja na uamuzi wa Spika kuhusu mgogoro wa gesi mkoani Mtwara.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema kuwa taarifa zinadhihirisha kwamba nchi imefika hali hiyo kutokana na udhaifu wa serikali na ombwe la kiuongozi na kiusimamizi ikiwamo wa kibunge.
Alisema kuwa taarifa ya waziri mkuu ilijibu baadhi tu ya madai ya wananchi lakini pia imefafanua sehemu ndogo ya masuala ambayo aliyahoji bungeni Julai 27, mwaka jana, lakini serikali ikakwepa kutoa ufafanuzi.
“Taarifa hiyo itawezesha kutuliza mgogoro kwa muda lakini haijengi msingi wa ufumbuzi endelevu. Sikubaliani na uamuzi wa spika wa kubadili uamuzi wake wa awali alioutangaza wa kuunda kamati kufuatia maelezo ya waziri mkuu yasiyokuwa na vielelezo vyovyote, kwa kuwa kufanya hivyo ni kulinyima Bunge fursa ya kuisimamia serikali ambayo ndiyo chanzo cha migogoro kuhusu gesi asili,” alisema.
Alisema kuwa ikiwa Spika amebadili uamuzi wa kuunda kamati ya kwenda Mtwara alipaswa aunde Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ili ipitie vielelezo kubaini usahihi wa maelezo hayo ya waziri mkuu bungeni katika hali ya sasa.
Mnyika aliongeza kuwa waziri mkuu hajatoa maelezo kamili kuhusu mipango ya matumizi ya gesi asili katika eneo la viwanda Bagamoyo na ujenzi wa Bandari ya Mbegani.
“Spika wa Bunge atumie mamlaka yake kuelekeza kamati mojawapo ya kudumu ya Bunge kushughulikia suala la gesi asili kama nilivyoomba katika barua zangu kwake za Oktoba 2012 na Januari 2013, ambazo hadi sasa hazijapatiwa majibu,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment