Zitto Kabwe
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitaendelea kufanywa
na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo itaendelea na jukumu lake
la msingi la kuchambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na kwa Serikaki Kuu.
Kamati nyingine iliyofutwa ni ya sheria ndogo, huku Spika akiunda kamati
mpya tatu na nyingine kuzifanyia marekebisho kadhaa ikiwa ni hatua ya
kuimarisha usimamizi wa Bunge kwa shughuli za Serikali.
Akitangaza mabadiliko hayo muda mfupi kabla ya kuahirisha mkutano wa
kumi jana, Makinda alizitaja kamati mpya kuwa ni Kamati ya Bajeti,
Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Kamati ya Ulinzi na
Usalama, ambayo imetenganishwa kutoka Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo
ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Kwa mujibu wa Spika Makinda majukumu ya kamati mpya ya bajeti ni
kufuatalia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, Sera za Fedha, kuanisha na
kupendekeza vyanzo vya mapato ya Serikali na kufuatilia mwenendo wa
uchumi.
Kamati hiyo pia imepewa jukumu la kushauri kamati nyingine zote kuhusu bajeti.
“Kwa sasa kuna baadhi ya kamati zinazosimamia wizara moja moja, ambazo
shughuli zake siyo nyingi ikilinganishwa na kamati nyingine
zinazosimamia wizara zaidi ya moja zikiwa na shughuli nyingi,”alisema
Makinda na kuongeza:
“Vivyo hivyo kuna wizara zinazohusika na kutunga sera, lakini kwa kiasi
kikubwa sera hizo zinatekelezwa na wizara nyingine hadi ngazi za chini.
Mfumo huu husababisha baadhi ya Kamati za Bunge kutoweza kufuatilia
vizuri utekelezaji wa shughuli za Serikali, kinyume na matakwa ya ibara
ya 63(3) ya Katiba na majukumu ya kamati yaliyoainishwa na Kanuni za
Bunge.”
Spika alifanya marekebisho hayo kwa mamlaka aliyopewa kwa kanuni ya 152 (3) cha Kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2007.
Kamati ambazo zimebadilishwa miundo yake ni ya Katiba, Sheria na
Utawala, Fedha na Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya
Ukimwi.
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara imeundwa na imepewa wajibu wa
kusimamia masuala ya uchumi, mitaji, uwekezaji, maendeleo ya viwanda na
shughuli za biashara.
Makinda alisema Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, imepunguziwa
majukumu na sasa itajikita kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya
Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na taasisi zake na Wizara ya Katiba
na Sheria.
“Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itasimamia utekelezaji
wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), pamoja na sheria ndogo
za halmashauri zote nchini,”alisema Makinda.
Alisema kwamba jukumu la Kamati ya Huduma za Jamii ni kufuatilia
utekelezaji wa Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi kwa ngazi ya elimu ya
Juu, Vyuo vya Ualimu, Elimu ya Ufundi (Veta) na taasisi za Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Pia Vyuo vya Elimu ya Juu vya Umma, Baraza la Mitihani, Taasisi ya
Kukuza Mitaala na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kamati hiyo pia
itasimamia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Spika alilieleza Bunge kuwa Kamati Nyingine ni ya Ukimwi na Dawa za
kulevya, ambayo imeongezewa jukumu la kufuatilia masuala ya matumizi ya
dawa hizo.
No comments:
Post a Comment