Msemaji wa Mkuu wa Polisi nchini, Advera Senso
Na: George Njogopa-Mwananchi
BOTI ya abiria iliyokuwa ikitokea Pangani mkoani Tanga kwenda Zanzibar ikiwa na watu 32 juzi usiku ilizama katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Zanzibar ambapo watu 10
wanahofiwa kuwa wamepoteza maisha.
Taaarifa
zilizofikia gazeti hili jana jioni zilisema kati ya abiria 27 na
wafanyakazi watano waliokuwa kwenye boti hiyo, ni watu 20 tu waliokuwa
wameokolewa wakati wengine 10 wakiwa hawajulikani walipo.
Msemaji wa Mkuu wa Polisi nchini, Advera Senso alisema jahazi liitwalo Sunrise liliondoka Tanga juzi saa 2:00 usiku kuelekea Zanzibar, lakini lilipigwa na dhoruba katika eneo la Nungwi.
“Mpaka sasa watu 22 wameokolewa akiwamo nahodha Abdallah Selemani, kumi wanatafutwa ijapokuwa wanahofiwa kuwa wameishakufa. Kati ya hao ni watoto watatu na watu wazima ni saba,”alisema Senso katika ujumbe alioutuma kupitia simu yake ya mkononi.
Aliendelea: “Boti kutoka Tanga ipo kwenye eneo la tukio kusaidia uokozi na wakazi wa Kaskazini Unguja wamepokea watu waliookolewa na kuwapa huduma. Taarifa zaidi tunaendelea kufuatilia Tanga na Zanzibar”.
Hata hivyo idadi ya watu waliookolewa kwa mujibu wa Senso ilitofautiana na ile iliyokuwa imetolewa awali na Kamanda wa Wanamaji na Bandarini Zanzibar, SP Martin Lisu aliyesema juhudi za kuwaokoa abiria hao zilikuwa zikiendelea na kwamba waliokuwa wamepatikana wakiwa hai ni watu 21.
Lisu
alisema abiria hao walionusurika kifo walipelekwa hospitalini kwa ajili
ya kuchunguzwa afya zao na wengine walipatiwa huduma za kwanza kutokana
na mshtuko walioupata.
“Kusema kweli tulifanikuwa kuwaokoa abiria 21 na wengine siwezi kusema kama wamezama ila nachoweza kusema ni kwamba bado hatujawapata,” alisema Kamanda Lisu na kuongeza:
“Taarifa nilizonazo ni kwamba, hii boti ilikuwa ikitokea Pangani, ilipofika eneo la Nungwi ikakubwa na dhoruba kali na kisha kuanza kupoteza mwelekeo”.
Eneo la Nungwi
Eneo la Nugwi lina historia ya kusababisha ajali za mara kwa mara na mara ya mwisho ndiko ilitokea ajali ya meli ya MV Spice Islander iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 400 mwaka 2011.
Eneo la Nugwi lina historia ya kusababisha ajali za mara kwa mara na mara ya mwisho ndiko ilitokea ajali ya meli ya MV Spice Islander iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 400 mwaka 2011.
Ajali hiyo ilielezwa kusababishwa na uzembe wa baadhi ya watendaji ikiwemo kukosekana kwa ukaguzi kabla ya meli hiyo kuondoka.Taarifa zilizema kuwa meli hiyo ilizidisha idadi ya abiria na mizigo hivyo ilipofika eneo la Nungwi ilizidiwa na kuanza kuzama.
Katika kujaribu kusaka ukweli wa mambo, Rais wa Zanzibar, Dk Ally Mohamed Shein aliunda tume maalumu kuchunguza mazingira yaliyosababisha ajili hiyo.
Ripoti ya tume hiyo ilifichua uzembe uliojitokeza kwenye mamlaka husika na kupendekeza hatua kadhaa ili kuimarisha hali ya usafiri kwenye maji.
Ajali nyingine kubwa ni ya meli ya MV Skagit iliyotokea mwaka jana ikiwa inakaribia katika bandari ya Zanzibar, ambayo hatua za awali za uokoaji zilishindikana na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
No comments:
Post a Comment