BAADA ya Televisheni ya Star TV kutangaza kujitoa kurusha matangazo yao kupitia kingamuzi cha Star Times, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema sheria na leseni ya huduma, inazuia kuchukua hatua hiyo.
Hata hivyo, TCRA imesema inafanya uchunguzi na leo itakutana na
uongozi wa Star TV na Star Times, kuzungumzia suala hilo ili hatua za
udhibiti, zichukuliwe kuwezesha wananchi kupata haki ya msingi ya kupata
matangazo ya kitaifa kupitia televisheni hiyo.
Star TV walitangaza kutoonekana kupitia Star Times siku chache
zilizopita. Uchunguzi wetu umebaini kuwa, jana
waliwasilisha barua ya hatua hiyo kwa kampuni ya Star Times kupitia
mwanasheria wa kampuni yao.
Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy aliliambia HabariLeo
jana kuwa na wao wamesikia taarifa hiyo kupitia vyombo vya habari
Lakini, alisema Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya
mwaka 2010, haitoi fursa kwa watu wenye televisheni kujitoa ama
kujiweka kwenye ving’amuzi watakavyo.
“Kwa ujumla chaneli zile tano za kitaifa, zinapaswa kuonekana bure
kwenye ving’amuzi vyote, nasi tumesikia habari hizi na lazima tufanye
uchunguzi, lakini pande zote mbili pamoja na sheria, pia wanafungwa na
mkataba wa huduma kwa jamii na matakwa ya leseni,” alisema Mungi na
kuongeza:
“Sheria inawataka wawe na makubaliano, huwezi kusema mimi
najitoa, leseni ina matakwa yake lazima yafuatwe. Lakini kesho (leo)
tutawaita kujua kilichotokea ni nini na hatua zaidi zitachukuliwa baada
ya hapo”.
Aliwahakikishia wananchi ni haki yao kupata matangazo kupitia
televisheni ya Star TV, hata bila kulipia ving’amuzi, kama ilivyo kwa
televisheni nyingine nne za ITV, TBC, Channel 10 na EATV.
Msaidizi wa Meneja wa Star Times, Hellen Elisa alithibitisha kujitoa
kwa Star TV. Alieleza ni kweli walipokea barua mbili juzi, zikieleza
kuhusu hatua yao hiyo kwamba wamejitoa kwa matakwa yao.
“Walituletea barua jana (juzi) kupitia mwanasheria wao wa kampuni,
wao ni wamiliki wa chaneli, na sisi tunahusika kurusha matangazo, jambo
lolote kama hili likitokea lazima kwanza kutii sheria, tumewasiliana na
TCRA na wakubwa wetu wa kazi wametueleza kuwa wanalishughulikia kwa
karibu,” alisema Elisa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa masuala ya Ving’amuzi wa Sahara Media
Group, wamiliki wa Star TV, Steve Diallo alipoulizwa kwa simu kuhusu
kujitoa kwao Star Times, alisema yeye si Msemaji na kumtaka mwandishi
kuwasiliana na watu wengine.
No comments:
Post a Comment