Timu ya
kuchunguza tukio la kutekwa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda (pichani), imebaini kuwa kazi
yake ya uandishi wa habari na siasa vimechangia kuvamiwa kwake na kuna
kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Aidha,
uchunguzi wa timu hiyo umebainisha kuwa baadhi ya watu waliohojiwa
walidai kuwa utekaji wa Kibanda ulifanywa na vyombo vya dola ukiwa
sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivyo kukihusisha Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vitendo vya ugaidi.
Taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo ilitolewa jana na
Mwenyekiti wa timu hiyo, Deodatus Balile, iliyoundwa na TEF katika
mkutano wa pili wa mwaka wa mashauriano kati ya Baraza la Habari
Tanzania (MCT) na jukwaa hilo jijini Tanga.
“Uchambuzi uliofanywa na timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa
kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:- Kazi yake
ya uandishi wa habari, Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa
mbalimbali, uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi na vitendo vya rushwa,”
ilieleza taarifa hiyo.
Alisema timu hiyo imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana
ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hilo kwani
waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba kushambuliwa na kuumizwa
Kibanda halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.
Imeeleza kuwa kazi yake ya uandishi wa habari na siasa vikiunganishwa
vimechangia kuvamiwa kwa Kibanda na kuna kutupiana mpira kati ya vyombo
vya dola na vyama vya siasa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa waliohojiwa waliyataja matukio ya uchaguzi
Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro ya Chadema na mkanda anaodaiwa
kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, kuwa
vililenga kukifanya chama hicho kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja
kama chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kuwaumiza.
“Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo
vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama
cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa
vyombo hivyo vililenga kukifanya Chadema kionekane cha kigaidi mbele ya
macho ya jamii, ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia
kujenga hoja hiyo,” taarifa hiyo ilieleza.
Aidha, baadhi ya watu waliohojiwa walidai kuwa Chadema kimepewa mafunzo
na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa
vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi
ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa, hivyo wananchi
wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kimeshindwa
uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.
Imeeleza kuwa kwa njia hiyo, hesabu za Chadema ni kuwa wananchi
wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani
na kauli ya Chadema kuwa nchi haitatawalika itakuwa imetimia.
Taarifa zaidi ya kamati hiyo imebainisha kuwa maisha ya wanahabari yapo
hatarini kutokana na makundi mengi yenye maslahi kuwaona wanahabari
wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa maslahi yao haramu.
“Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015,” taarifa hiyo ilisema.
Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari tofauti
na zamani wakati ambao habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya
waandishi wakitumia jina la Mwandishi wetu, lakini siku hizi hata
habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka,
ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani
ameandika habari fulani.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe
ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali
itazidi kuwa mbaya zaidi.
Taarifa hiyo inamnukuu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya
Habari nchini (MOAT), Dk. Reginald Mengi akisema: “Hili ni jambo muhimu
sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi wataumia.”
Taarifa ya kamati hiyo inabainisha kuwa mazingira ya kazi ndani ya
Kampuni za New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha
maswali kadhaa yenye kustahili majibu na ndani ya New Habari kumekuwapo
na misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia
ya habari kwa ujumla.
“Mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si mzuri.
Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa
huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na
kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai
kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo alihusika na utekaji wa
Kibanda, uchunguzi huo umebainisha.
Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari
(2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’.
Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na
watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.
“Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi
kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa
Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe, alianza kumsikiliza zaidi
msaidizi wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo
kuliko yeye Kibanda.”
Kibanda alitekwa usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, mwaka huu
na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake
eneo la Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, Kibanda aliumizwa kwa kutobolewa jicho la kushoto,
akaumizwa kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa
ya kichwa.
Aidha watekaji walimng’oa meno mawili na kucha mbili, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.
Wakati timu hiyo iliyowashirikisha Balile, Pili Mtambalike , Jane
Mihanji, Tumaini Mwailenge na Rashid Kejo ikiwasilisha taarifa yake,
timu iliyoindwa na jeshi la Polisi kuchunguza tukio hilo hadi sasa
haijafanya hivyo, badala yake imekuwa ikisisitiza kuwa uchunguzi
unaendelea.
habari NA THOBIAS MWANAKATWE
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment