Pages


Photobucket

Saturday, June 8, 2013

Katiba Mpya yang'oa vyama meno


Ile ‘nyundo’ inayotumiwa kuwashughulikia wabunge wanaotokana na vyama vya siasa, inaelekea kuzikwa rasmi, baada ya Rasimu ya Katiba mpya ya mwaka 2013, iliyozinduliwa Jumatatu wiki hii, kupendekeza kwamba uamuzi wa vyama hivyo wa kuwafukuza au kuwavua uanachama, hautapoteza ubunge wao. Vyama vya siasa vitang’olewa meno rasmi ikiwa rasimu hiyo iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, itapitishwa na Watanzania na kuwa Katiba rasmi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pendekezo hilo linaelezwa bayana na ibara ya 123 kifungu cha (2) cha Rasimu hiyo ya Katiba mpya.
Kifungu hicho kinaeleza: “Mbunge aliyependekezwa na chama cha siasa, hatapoteza Ubunge wake ikiwa Mbunge huyo atafukuzwa au kuvuliwa uanachama wa chama chake,” kinaeleza kifungu hicho cha Rasimu ya Katiba mpya.
Hata hivyo, kifungu kinachofuata cha (3) kilichopo katika ibara hiyo (ya 123) ya Rasimu hiyo ya Katiba mpya kinapendekeza namna mbunge atakavyopoteza ubunge wake.
Kifungu hicho kinaeleza: “Endapo mbunge, kwa ridhaa yake atajiondoa au kujivua uanachama kutoka chama chake cha siasa, Mbunge huyo atapoteza sifa za kuwa Mbunge na atasita kuwa Mbunge.”
Tofauti na pendekezo la Rasimu hiyo ya Katiba mpya, Katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977 inaelekeza sifa za mtu kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge kwamba, ni pamoja na kuwa mwanachama wa chama cha siasa.
Maelekezo hayo ya Katiba ya sasa yanatolewa kwenye ibara ya 67 kifungu cha (1) sehemu (b).
 Kifungu hicho kinaeleza: “Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge:-
“Endapo ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.”
Aidha, Katiba ya sasa inaelekeza kuwa mbunge hatakuwa mbunge iwapo pamoja na mambo mengine, hatakuwa mwanachama wa chama cha siasa. 
Hilo linaelekezwa na ibara ya 71 kifungu cha (1) sehemu (f) ya Katiba hiyo inayotumika sasa.
Kifungu hicho kinaeleza: “Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge litakeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:-
“…Iwapo Mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge.”
Mapendekezo hayo ya Rasimu ya Katiba mpya, yametolewa, huku kukiwa na kesi zilizofunguliwa na wabunge wawili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga kuvuliwa uanachama na vyama vyao.
Wabunge hao; ni Hamad Rashid Mohammed (Wawi-CUF) na David Kafulila (Kigoma Kusini-NCCR-Mageuzi).
Wabunge hao walifungua kesi hizo kwa nyakati tofauti mwaka jana wakipinga maamuzi yaliyochukuliwa na vyama vilivyowapa tiketi ya kuwania ubunge, kuwavua uanachama kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Pia waliokuwa wabunge Erasto Tumbo (Kisesa-UDP) na Danhi Makanga (Bariadi Mashariki-DP) waliwahi kukumbwa na mkasa wa kuvuliwa uanachama na chama chao cha siasa cha United Democratic (UDP) na hivyo, kupoteza ubunge katika miaka ya 2000.
 Wengine ni waliokuwa wabunge wa viti maalum kupitia Chama cha Wananchi (CUF); Naila Majid Jidawi, Zamda Bozen (Tabora), Aisha Filipo (Pwani), Adela Stela Mkilindi (Tanga) na Asha Ngede (Dodoma), walivuliwa uanachama mwaka 2001 na kulazimika kukimbilia mahakamani kuweka pingamizi dhidi ya maamuzi ya chama chao.
Wote walikumbana na mkasa wa kuvuliwa uanachama baada ya kukataa kutii amri ya chama kilichotaka wasusie vikao vya Bunge ili kuungana na wabunge wenzao wa CUF kutoka Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliamua kususia vikao vya Baraza ili kushinikiza kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2000 baada ya aliyekuwa mgombea urais visiwani humo kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuporwa ushindi wake katika uchaguzi huo na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Amani Abeid Karume. 
Mwingine ni aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini kupitia Chama cha Tanzania Labour (TLP), Thomas Ngawaiya,  katika miaka ya 2000 naye pia aliwahi kutimuliwa na chama chake na hivyo, kujikuta akipoteza ubunge. 
Hata hivyo, Ngawaiya alipinga hatua hiyo mahakamani na baada ya Bunge la mwaka 2000 kumaliza uhai wake, Ngawaiya alikihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
MIKOA KUWA MAJIMBO
Tofauti na inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotumika sasa ya mwaka 1977, Rasimu ya Katiba mpya inapendekeza kwamba, kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa ni jimbo la uchaguzi.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, katika kila jimbo la uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za ubunge, moja ya kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamume.
Aidha, rasimu hiyo inapendekeza kuwa wabunge wote katika kila jimbo la uchaguzi watapatikana kwa kupigiwa kura na wananchi.
Mapendekezo hayo yanatolewa na rasimu hiyo ya Katiba mpya katika ibara yake ya 105 kifungu cha (3), (4) na (5).
Vifungu hivyo vinaeleza: “Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (2) (a), kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa ni jimbo la uchaguzi.”
“Katika kila Jimbo la Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamume.”
“Wabunge wote katika kila Jimbo la Uchaguzi watapatikana kwa kupigiwa kura na wananchi kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria inayoweka utaratibu kuhusu mambo ya uchaguzi.”
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotumika sasa ya mwaka 1977, haielezi mipaka ya majimbo ya uchaguzi.
Badala yake, katika ibara ya 75 kifungu cha (1) hadi kifungu cha (5) na ibara ya 6, imeishia tu kuipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya kuweka mipaka ya majimbo ya uchaguzi baada ya kupata kibali cha Rais, na kuizuia mahakama kuingilia utekelezaji huo wa NEC.
Upande wa Tanzania Bara, kuna jumla ya mikoa 25; minne kati yake ikiwa ni mipya.
Mikoa hiyo ni Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Tabora, Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Pwani, Mbeya, Manyara na Iringa. 
Mikoa minne mipya inayotimiza idadi ya mikoa 25 iliyoko Tanzania Bara, ni Katavi, Njombe, Simiyu na Geita.
Rasimu ya Katibu mpya inapendekeza kuwapo wabunge 75; kati yao, 50 kutoka Tanzania Bara, 20 Zanzibar na watano watakaoteuliwa na Rais kutoka makundi maalum ya watu wenye ulemavu.
Hivyo, ikiwa Rasimu hiyo ya Katiba mpya itapitishwa na Watanzania, mtu atakayeamua kugombea ubunge, atalazimika kuzunguka mkoa wote kutafuta kura za wananchi, badala ya jimbo, ambalo liko sehemu ya mkoa. 
 habari nA MUHIBU SAID
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment