Pages


Photobucket

Wednesday, June 26, 2013

AJALI ZA BODABODA NI JANGA LA TAIFA: KUWENI MAKINI NA BODA BODA ZENU:




Matukio ya kasi kubwa ya ajali za pikipiki nchini zinazogharimu maisha ya watu wengi yameitisha serikali na kuamua kutoa tamko bungeni kueleza ukubwa wa tatizo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, jana alitoa taarifa ya serikali bungeni kuhusiana na tishio hilo na kusema kuwa bila hatua za dhati na za haraka kuchukuliwa, taifa litazidi kuangamia.
Dk. Nchimbi aliliambia bunge kuwa watu 352 wamepoteza maisha na wengine 2,368 kujeruhiwa kutokana na ajali za pikipiki zilizotokea kati ya Januari hadi Mei mwaka huu nchini.
Alisema kutokana na idadi ya vifo na majeruhi kuwa kubwa, hospitali nyingi zimeamua kuanzisha wodi maalum za majeruhi wa pikipiki.
“Matumizi ya pikipiki nchini yamesababisha ongezeko kubwa sana la ajali za barabarani ambazo zimegharimu maisha ya Watanzania wenzetu wengi sana,” alisema.
Alisema pamoja na upotevu wa maisha, ajali hizi zimewasababishia ulemavu wa kudumu watu wengi kwa kupoteza viungo vyao na kuwafanya kuwa tegemezi.

Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, mkoa wa Dar es Salaam ambao una jumla ya pikipiki 4,432, unaongoza kwa kuwa na ajali 2,161 zilizosababisha vifo 56 na majeruhi 1,211.

Alitoa  mchanganuo wa idadi za ajali hizo kwa wilaya za Jiji la Dar es Salaam kuwa ni, Kinondoni 515 na vifo vilivyotokea ni 22 na majeruhi 549; Temeke ajali zilikuwa 299, vifo 19 na majeruhi 354 wakati Ilala ajali ni 357, vifo 15 na majeruhi 307.
Aliitaja mikoa mingine yenye ajali nyingi kuwa ni Morogoro uliokuwa na ajali 186, vifo 15 na majeruhi 117, wakati Arusha kulikuwa na ajali 118, vifo 16  na majeruhi 102.
Mikoa mingine ni Kilimanjaro ajali 130, vifo 26 na majeruhi 120, wakati Pwani ajali zilikuwa 114 na kusababisha vifo 23 na majeruhi 167.
“Tusipochukua hatua za makusudi taifa letu litaendelea kuathirika na ajali hizo ambazo zinachukua maisha ya watu wetu na kuongeza idadi ya yatima, walemavu na watu wasiojiweza na kuwafanya wawe tegemezi,” alisema.
Alisema idadi ya ajali, vifo na majeruhi nayo inazidi kuongezeka siku hadi siku kwa kadri pikipiki zinavyoongezeka.
“Ukitazama takwimu nilizozitoa awali, utagundua kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya idadi ya pikipiki na ajali zinazotokea,” alisema.
Dk. Nchimbi alisema yapo maeneo ambayo yana pikipiki chache, lakini uwiano wa pikipiki na ajali zinazotokea ni mkubwa sana.
“Kwa takwimu hizi ni wazi tunalo tatizo kubwa katika sekta ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia pikipiki,” alisema na kuwaomba wabunge wasaidie katika kuhamasisha vijana hasa madereva wa bodaboda kuhakikisha wanapata mafunzo ya udereva.
Dk. Nchimbi alisema vyanzo vya ajali hizo ni pamoja na kutojua sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya barabara na kwamba madereva wengi hawana leseni za udereva.
Sababu nyingine ni madereva wa magari kutoheshimu wapanda pikipiki na kujenga mtazamo hasi dhidi yao kwamba wanaendesha kwa fujo pamoja na baadhi ya barabara kukosa alama ama alama zilizofifia ambazo siyo rahisi kuonekana.
Nyingine ni uendeshaji wa hatari wa pikipiki barabarani kwa kwenda mwendo wa kasi, kupita katika taa za kuongezea magari bila kuruhusiwa, kudharau trafiki, kupakiza idadi kubwa ya abiria na matumizi ya vilevi.
Dk. Nchimbi alisema mikakati mbalimbali inafanywa na Jeshi la Polisi katika kukabiliana na wimbi kubwa la ajali za pikipiki.
Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni usimamizi na udhibiti kwa watoaji na watumiaji wa usafiri huo ambao unafanywa kwa kutumia kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) za mwaka 2010 zinazohusu usafirishaji wa abiria kwa kutumia pikipiki.
Mkakati mwingine ni kuwatumia waendesha pikipiki kutoa taarifa za uhalifu na makosa wanapoona wenzao wanakiuka taratibu na kuandaa operesheni mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa waendeshaji wa pikipiki wanaofuata sheria katika uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni halali.
“Mikakati mingine ni kuhakikisha upakiaji salama wa abiria, matumizi ya kofia ngumu (helmet) na uendeshaji wa kujiami, utoaji wa elimu kwa kutumia vyombo vya habari kama redio, televisheni na magazeti na kuandaa vipeperushi vya elimu kwa waendesha pikipiki,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yanafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama asasi zisizo za kiserikali na vyuo vya udereva hususani Mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta).
Alitaja mikakati mingine kuwa ni utoaji elimu kwa kushirikisha waendeshaji pikipiki katika michezo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment