Mbunge wa
kuteuliwa, James Mbatia ameitaka Serikali isiishie kuivunja Kamati ya
Ithibati ya Vifaa vya Elimu, (EMAC), na badala yake iende mbali zaidi
kwa kuwachukulia hatua za kisheria wajumbe wote wa kamati hiyo. Mbatia
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi alisema jana mjini
Dodoma kuwa kamati hiyo inahusika moja kwa moja kuua elimu nchini
kutokana na kufumbia macho ufisadi ulioruhusu kusambazwa kwa vitabu
visivyo na ubora.
“Hawa
ni wahujumu uchumi wa nchi yetu; wanahusika kuididimiza elimu yetu...
Inaonyesha wazi kuwa watunzi wa vitabu vile hawakutumia mitalaa.
Kutokuongozwa kwa mitalaa kumesababisha vitabu vile kukosa ubora.
Haiwezekani mwandishi, mhariri na mhakiki, awe mtu mmoja.” alisema.
Mbatia
alisema Emac imetoa ithibati kwa vitabu vyenye maudhui yasiyo sahihi au
dhaifu na ambayo hayamo kwenye mihutasari huku baadhi yao vikiwa
vimeiwakilisha vibaya Bendera ya Taifa pamoja na Nembo ya Taifa kwenye
baadhi ya vitabu hivyo.
Alisema
miongoni mwa vitabu vilivyopitishwa na Emac havina majina ya waandishi
na kwamba badala ya jina la mwandishi limewekwa jina la kampuni ya
uchapishaji.
“Hakuna hata
kitabu kimoja chenye wasifu wa mwandishi na karibu vitabu vyote havina
wahariri wakati ni lazima kila kitabu kiwe na angalau mhariri mmoja”
alisema Mbatia.
Alisema
kasoro nyingine iliyopo katika vitabu hivyo ni makosa mengi ya lugha
iliyotumika kuandikia ambayo ni Kiswahili, hali inayoonyesha kuwa vitabu
hivyo havikupitishwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).
“Aibu
nyingine ipo katika maelezo ambapo eti wameandika mitalaa ya shule za
awali unamwezesha mwanafunzi kukua kiuchumi, kisiasa na kijamii…na kwa
wale wa shule ya msingi, wanasema mtalaa unamsaidia mwanafunzi kupata
uelewa wa lugha ya Kifaransa ili aweze kupata ajira…Kweli mwanafunzi wa
shule ya awali anatakiwa akue kiuchumi, kisiasa na kijamii….na hii lugha
ya Kifaransa inatoka wapi katika mtalaa wa Tanzania” alihoji Mbatia.
Mbatia
aliitaka Serikali vilevile iviondoe sokoni vitabu vyovyote vya kiada na
ziada vyenye maudhui potofu kama inavyofanya kwa bidhaa nyingine zisizo
na ubora.
“Adhabu
zitolewe kwa watayarishaji na wamiliki wa vitabu duni vitakavyoingizwa
shuleni kinyume na taratibu ili kuzuia matendo ya rushwa…chombo cha
kupokea taarifa kutoka kwa wadau wa elimu kuhusu vitabu duni kiundwe”
alisema.
Alisema
endapo Serikali itapuuza na kuviacha vitabu hivyo visivyo na ubora
kuendelea kutumika, ubora wa elimu utazidi kuporomoka kwa sababu
wanafunzi watalazimika kutumia vitabu visivyo na ubora
Habari na Joyce Mmasi,
Chanzo - Mwananchi
No comments:
Post a Comment