Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema ina ushahidi
unaoonyesha njama za kuhakikisha kuwa ni wana CCM pekee, ndiyo
watakaochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande
wa Tanzania Bara.
Imedai kuwa njama hizo zimepangwa na ngazi za juu za chama hicho.
Akitoa maoni upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi ya
Upinzani kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema Machi
3, mwaka huu siku mbili baada ya Mwongozo wa Tume kuanza kutumika,
Katibu wa NEC ya CCM (Uhusiano wa Kimataifa), Dk Asha-Rose Migiro
alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC-CCM
inayoonyesha kujipanga kuingia kwenye mabaraza peke yao.
“Barua pepe ya Dk Asha-Rose Migiro inasema
“Sambamba na hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya
mwanzo ya Mwongozo wa Tume, sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki
wetu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea,” Lissu
alinukuu barua pepe hiyo.
Lissu alisema baada ya Dk Migiro kuagiza
alimalizia kwa maneno yafuatayo: “Tafadhali wanakiliwa msisite kutoa
maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala
hili muhimu.”
Aliwataja waliopelekewa nakala ya barua pepe ya Dk
Asha-Rose Migiro, kuwa ni Mwigulu Nchemba, Zakhia Meghji, Muhammed Seif
Khatib na Nape Nnauye.
Lissu alisema siku moja baadaye, Nape aliwaandikia
‘wanakiliwa’ wenzake akiwashauri ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa
suala hilo, wapate taarifa kila siku kuhusu hali halisi inavyoendelea
katika kila mkoa na kwamba ni vizuri idara ikaandaa orodha ya mambo
muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda vizuri au la!
Alisema njama za CCM kuteka nyara mchakato pia
zinahusu uhalalishaji wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni na kwamba,
Desemba 18, mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM, Francis Mwonga, aliwaandikia barua makatibu wote wa CCM wa
mikoa na kuwapa maelekezo ya kikao cha Sekretarieti.
“Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya
mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe
mbali sana na wananchi,” alisema Lissu akimkariri Mwonga.
Lissu alisema maneno hayo yaliandikwa hata kabla
Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, tayari
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani,
kufanya mawasiliano na ‘wahusika’ kuhusu jinsi ya kupanga vituo vya
kupigia kura.
Alisema mawasiliano hayo ya viongozi wa ngazi za
juu za CCM, yanathibitisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya umeingiliwa na
kuhujumiwa kwa kiwango kikubwa na CCM.
Pia, alisema mawasiliano hayo yanathibitisha kauli
iliyotolewa bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wakati wa
mjadala wa hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba viongozi wa Serikali
walihamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kuwa
wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa Chadema wanaenguliwa chaguzi za
vijiji, mitaa au kata.
Washtukia bajeti Tume ya Katiba Mpya
Tume hiyo iliombewa kuidhinishiwa Sh33.944 bilioni
sawa na kiwango kilichoidhinishwa mwaka jana, kwa ajili ya matumizi
mwaka 2013/14, Sh2.193 bilioni kwa ajili ya kulipia posho za vikao kwa
wajumbe 34 na 160 wa sekretarieti.
Lissu alisema Sh1.728 bilioni zitalipia posho ya
kujikimu kwa ajili ya wajumbe na sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi
na Sh1.650 bilioni kwa ajili ya kulipa gharama za nyumba kwa wale
wanaotoka nje ya Dar es Salaam.
Mbunge huyo alisema kuna Sh18 milioni zinazoombwa
kugharamia chakula kwa wajumbe wa tume na sekretarieti watakaokuwa
wamepata maambukizi ya Ukimwi.
Pia Sh60 milioni kwa ajili ya usafiri wa ndani,
Sh50 milioni gharama za malazi kwa wajumbe wa tume na sekretarieti
wanaposafiri kikazi.
“Sh423 milioni za chai na vitafunwa na Sh50
milioni za wahudumu wanaosaidia kazi za tume wakiwa mikoani wakati wa
kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni,”
alisema.
Alisema Sh60 milioni zinatakiwa kulipia maji kwa
matumizi ya ofisi za tume, Sh30 milioni za kulipia gharama za usafiri wa
basi na teksi kwa wajumbe na sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi
kikazi na Sh103 milioni za kulipia gharama za simu za mikononi.
“Ulaji huu mwingine unajumuisha Sh604 milioni za
posho kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wakati wa Bunge Maalumu la
Katiba. Maelezo ya tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za
ziada kwa kuzibatiza jina la ‘hardship allowances’, yaani posho ya
mazingira magumu, wakati vikao vya Bunge Maalum la Katiba vitafanyika
Dar es Salaam au hapa Dodoma!” alisema.
Pia, alisema kwenye ulaji huo mpya kuna Sh266
milioni za chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalum la
Katiba na Sh12 milioni kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa
shughuli zinazohusiana na Tume.
Hali kadhalika Sh185 milioni za usafiri wa basi na
teksi na Sh30 milioni za kutengeneza fulana na kofia kwa wajumbe wa
tume na sekretarieti.
“Sh19.039 bilioni zinaombwa kwa ajili ya posho za
aina mbalimbali na malipo mengine yanayowahusu wajumbe na sekretarieti
ya tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Hii ni zaidi ya asilimia 56 ya
bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya tume.
Kwa ulinganisho, posho na malipo mengine
yanayowahusu wajumbe na sekretarieti ya tume yalikuwa Sh14.633 bilioni
au asilimia 43 ya bajeti yote ya mwaka wa fedha uliopita,” alisema Lissu
na kuongeza:
“Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za wajumbe na sekretarieti ya tume zitaongezeka kwa zaidi ya Sh4.406 bilioni au zaidi ya asilimia 30 ya gharama za mwaka jana kama Bunge litaidhinisha maombi haya,” alisema Lissu.
“Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za wajumbe na sekretarieti ya tume zitaongezeka kwa zaidi ya Sh4.406 bilioni au zaidi ya asilimia 30 ya gharama za mwaka jana kama Bunge litaidhinisha maombi haya,” alisema Lissu.
No comments:
Post a Comment