Kwa
mliotaka msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa jana tarehe 18 Julai
2013 na Gazeti la Majira kwamba Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia Januari Makamba kwamba; “Mnyika anaangalia upepo unakoelekea,
akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa
katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao huu kutoa majibu ya ujumla
kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:
Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo
itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha
walau kidogo kwa maendeleo.
Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu ambayo wananchi
walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali ambayo
yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu
Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi
na uongozi bora.
Ambacho sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za
kusema uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea
kuhusu suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili
nilianza kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha
kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu
ikiwemo hii. Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa
sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada
wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.
Aidha, sikuishia kusema tu kwa niaba ya wananchi bali nilichukua hatua
kwa mujibu wa kanuni za Bunge nami kuwasilisha jedwali la marekebisho ya
kupinga kodi ya umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine zote
zenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi sio kwenye sekta
ya mawasiliano bali pia kwenye sekta zingine ikiwemo sekta ndogo (sub
sector) nyeti ya mafuta.
Mlioniuliza kwa SMS katika simu na kwenye mitandao ya kijamii sasa ni
wakati wa Makamba kuhojiwa kwa njia hizo hizo (Simu yake ya Mkononi ni
0767783996) kwa kuwa yeye ni sehemu ya Serikali na Serikali ndiyo ambayo
iliingiza suala hili kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge
kupitia hotuba ya Bajeti Serikali na ikalirudia kuliingiza kupitia
jedwali la marekebisho ya Sheria ya Serikali; ni wakina nani hasa kwa
majina ndani ya Serikali na Bunge walioingiza kodi hii? Na ni wakina
nani hasa waliopigia kura ya ndio kuipitisha?
Aidha, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo tarehe 19 Julai 2013
akieleza kwamba hakubaliani na suala hili na kupita kwake ilikuwa na
kuzidiwa nguvu. Hivyo, ataje kwa majina hayo waliozidi nguvu serikali
kinyume na matakwa yake. Amenukuliwa akisema pia kwamba anajua kuwa
suala hili haliwezi kutekelezwa na kwamba ni lazima litabadilishwa kwa
kuangalia eneo lingine la kutoza kodi. Ni vizuri akahojiwa, ikiwa huo ni
msimamo wa Serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha kodi hiyo ni nani na
kwanini hajitokezi kutoa agizo la kusitisha wakati maandalizi
yakiendelea ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa kodi hiyo
katika mkutano ujao?
Wakati Naibu Waziri akisema hayo, Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa
katika Serikali hiyo hiyo yeye ametoa kauli tofauti siku hii hii ya leo
ambapo kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao
ya simu nchini na watanzania kwa ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya
sh 1000 kwa mwezi kwa kila laini ya simu za kiganjani.
Na kwa kuwa amesema kwamba Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa
wadau, natoa mwito kwa wananchi kumtumia maoni kupitia namba zake za
simu za mkononi 0754/0684-765644. Aidha, ni vizuri aeleze subira hiyo
ivutwe mpaka lini? Na ni wakina nani hasa kwa majina waliomfanya
akaingiza kodi hiyo katika kitabu cha Hotuba yake aliyosoma bungeni
kuhusu bajeti ya Serikali na wakina na hasa kwa majina waliomfanya
arejeshe kodi hiyo ya kadi za simu kwenye jedwali la marekebisho ya
muswada wa sheria ya fedha alilowasilisha bungeni.
Nasisiza kuwa kauli za ujumla za Serikali bila kuwataja kwa majina
wahusika ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi
kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge. Ni
muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Rais ama
kiongozi mwingine mwenye mamlaka ajitokeze kusitisha kutozwa kwa kodi
hiyo na kuanzisha mchakato wa muswada wa kufuta kodi hiyo kuwasilishwa
katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 27 Agosti 2013.
Majina ya wahusika yasipotajwa au mamlaka zinazohusika zisipotoa kauli
katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki jumapili tarehe 21 Julai 2013
katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11
Jioni nitatoa mrejesho kuhusu yaliyojiri katika mkutano uliopita wa
Bunge na kueleza hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa kuwezesha majina ya
wabunge hao kutajwa hadharani na hatua za kuondoa kodi hiyo
kuchukuliwa.
Uongozi bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya
ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi.
Twende kazi.
John Mnyika (Mb)
19 Julai 2013
No comments:
Post a Comment