Na Editha Majura, Mwananchi
Wajumbe 96 wa Mabaraza ya Katiba, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, wamekutana kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, kwa lengo la kuiboresha, kazi itakayodumu kwa siku tatu.
Akifungua mkutano huo jana, Afisa Utumishi wa
wilaya hiyo, Donard Nssoko, alitaka wajumbe hao watoe maoni kwa niaba ya
wananchi ili Katiba ijayo iwe yenye maslahi kwa vizazi vya sasa na
vijavyo.
Katika hali inayoashiria kuwa, tume imedhamiria
kudhibiti wajumbe wa mabaraza hayo,wasiingize maoni yanayotokana na
shinikizo la makundi ya kisiasa, kidini na kiuana harakati, mbinu
mbalimbali za kubadili fikra za wajumbe hao zilitawala ufunguzi wa
mkutano huo.
Mwenyekiti wa Tume mkoani humo, Dk, Sengondo
Mvungi aligeuka muhubiri alipokuwa akielekeza namna wajumbe
wanavyotakiwa kutekeleza jukumu hilo, baada ya maelezo yake kulenga
kujenga hofu ya Mungu ndani ya wajumbe.
“Mmetumwa na wananchi siyo mjigeuze tume, bali
mboreshe maoni yao kwa kuandika kila kitakacholetwa na mjumbe, ili
kikafanyiwe kazi na tume; kushiriki kwenu kuunda sheria kuu kwa
Watanzania siyo suala la kibinadamu, bali Mungu amekushirikisha ufanye
kazi hiyo kwa niaba yake,” alieleza Dk, Mvungi
Dk. Mvungi aliwataka watambue kuwa hawapo kutumiwa
na makundi fulani, kuchakachua kwa kubadili maoni ya wananchi yaliyo
katika rasimu, bali kuyaboresha na kwamba kama ilivyo kwa imani za
Kikristo na Kiislamu, kwamba wanaoshiriki kujenga Kanisa au Msikiti
wamebarikiwa.
Alisema kidunia, wanaoshiriki kuunda Katiba ambayo
ni sheria kuu ya nchi, wamebarikiwa na kwamba kinyume na baraka za
Mungu ni laana, hivyo akaasa wanapotekeleza jukumu hilo, wajitambue kuwa
wanamtumikia Mungu kwa ajili ya watu wake wa Tanzania.
“Mimi siyo Padri, Askofu wala Sheikh nakuelekeza
haya, ili ufahamu kuwa usipokuwa mwaminifu kwa Mungu na taifa lako
katika hili, hutapata nafasi ya kujitetea mbele za Mungu, msije mkasema
hatukujua kuwa kazi ya kutunga Katiba ni ya Mungu; ukikosea
utahukumiwa,” Dk. Mvungi alieleza
Mjumbe wa Sekretalieti ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Marlin Komba kabla ya kufungua mkutano huo, alitoa karatasi kwa
kila mjumbe ili iandike wadhifa na sifa yake katika jamii aliyotoka.
Vikakusanywa na kuhifadhiwa kwenye bahasha moja.
“Vyeo na sifa zenu zimehifadhi kwenye bahasha hii,
ukumbini mmebaki wajumbe wa mabaraza ya Katiba, mtakaoboresha rasimu ya
Katiba ili ipatikane Katiba itakayokidhi mahitaji ya Watanzania siyo
kwa maslahi ya dini, siasa au uanaharakati,” Komba alieleza
Kama hiyo haitoshi, mwisho wa maelekezo ya tume,
Komba aliongoza mabaraza hayo kuimba ubeti mmoja wa wimbo wa taifa,
akihimiza kuzingatia umuhimu wa kumshirikisha Mungu na kuzingatia utaifa
katika kazi wanayotakiwa kufanya.
Baadhi ya wananchi walionekana kupendelea zaidi
makundi fulani ya wananchi, mambo ambayo yanaonekana wazi kwamba
yanaweza kuifanya katiba isizae matarajio ambayo wengi wanayo ya kuwepo
kwa katiba iliyo safi kwa wote.
No comments:
Post a Comment