Dodoma.Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amevunja ukimya na kusema yuko tayari kuachia ngazi endapo tu Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo, atamshukuru Rais kwa kumwambia, ahsante.
Pinda aliliambia Bunge mjini Dodoma jana kwamba
endapo Rais hatafanya hivyo, bado wabunge wanayo mamlaka ya kikatiba ya
kumwondoa kwa njia ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa
na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika utaratibu wa
Bunge wa Waziri Mkuu kujibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.
Katika swali lake, Mbunge huyo alisema; Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa akiwa jijini Mbeya kuwa wapo
mawaziri mzigo katika Baraza la Mawaziri.
Mbunge huyo alisema, katika ziara hiyo, Kinana
alifuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa NEC
ya CCM, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro.
“Walipokuwa Mbeya wakifuatilia utekelezaji wa
Ilani ya CCM, Kinana alisema kuna baadhi ya mawaziri ni mzigo, wewe kama
kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali unachukuliaje kauli hii?”
aliuliza.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata yeye
ameyasikia hayo kwenye vyombo vya habari na kusema, kiutu uzima hawezi
kutoa maoni yake kwa kuzingatia yale yanayosemwa kwenye magazeti.
“Sisi tunangoja arudi (Kinana) tukae naye ili
tujue alichokuwa anasema hasa ni nini na ninaamini alikuwa na baadhi ya
wizara kichwani kwake,” alisema Pinda bungeni jana.
Katika swali lake la nyongeza, Rukia alisema
wakati wanachangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, yupo
Mbunge wa CCM alisema kuwa Pinda ni mzigo namba moja.
“Kuna mbunge, tena wa CCM, alinukuu kauli ya
Katibu Mkuu wa CCM na akasema kama ni mawaziri mzigo basi mzigo nambari
moja ni wewe Waziri Mkuu, unawaambiaje Watanzania?” aliuliza Rukia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia
wizara 20 hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa wizara moja ama mbili kwa
kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Na MWANANCHI
Na MWANANCHI
No comments:
Post a Comment