Serikali ya Jamhuri ya
kidemokrasia ya Congo hatimaye imesaini mkataba wa amani na waasi wa
kundi la M23 waliokuwa wakifanya mashambulio ya mara kwa mara mashariki
mwa nchi hiyo.
Waasi wa M23 walijilsalimisha mwezi uliopita
baada ya kushindwa katika oparesheni iliyoendeshwa na serikali ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikisaidiwa na majeshi ya Umoja wa
Mataifa. Alhamisi, marais Yuweri Museveni, ambaye ndiye mwenyekiti wa
kongamano la kimataifa juu ya usalama katika maziwa makuu, na Joyce
Banda, rais wa Malawi, ambaye ndiye mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo
ya kusini mwa Afrika SADC, walisaini kama wadhamini wa mkataba huo.
Marais hao walisaini mkataba huo wakiwa jijini Nairobi walikohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Kenya.
Makubaliano
- Kundi la M23 limeweka rasmi katika mkataba huo kuwa watasitisha maasi yote na kulivunja kundi lao kama vugu vugu la waasi na badala yake kusukuma ajenda zake kupitia njia za kisiasa.
- Serikali ya Congo nayo imeweka masharti ya kutolewa msamaha kwa waasi hao na mpango wa kupokonywa silaha wote wanaojisalimisha kutoka kwa kundi hilo.
- Serikali hiyo pia imekataa kuwajumuisha kijumla waasi wote waliojiondoa kutoka M23, katika jeshi lake.
Safari ndefu
Juhudi za awali kutafuta amani kati ya serikali
ya DRC na waasi hao wa M23 zilishindikana. Mwaka mzima baadaye, licha ya
kuandikwa mkataba huo, pande mbili zilikataa kusaini kutokana na
kushindwa kukubaliana jina litakalopewa. Upande wa serikali ya DRC
ulisisitiza kuwa hakuna mkataba wa amani na waasi, hasa baada ya kuwa
wamewashinda vitani.
Tangu kupigwa na kufukuzwa kwa waasi hao kutoka
mkoa wa Kivu ya kaskazini, waasi hao wa M23 wamekuwa wakijisalimisha kwa
serikali ya Uganda na kuomba hifadhi. Serikali ya DRC imetaka
warudishwe nchini humo ili wakabiliwe na mashtaka ya mauaji, ubakaji na
uhalifu mwinigne wa kivita. Hata hivyo Uganda imekataa kuwakabidhi
ikisema kuwa ni wakimbizi wanaosubiri uamuzi kutoka shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia wakimbizi,UNHCR.
Hadi sasa amani imeanza kurejea katika maeneo
yaliyokombolewa kutoka mikono ya waasi wa M23. Hata hivyo mwandishi wa
BBC katika eneo hilo Lubunga Bya Ombe, anasema kuwa bado serikali hiyo
ya DRC ina kibarua kigumu kukabili makundi mengine madogo ya waasi
yaliyo kita kambi katika eneo hilo.
Wiki hii serikali ya DRC ikishirikiana na kikosi
cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa imetangaza oparesheni mpya dhidi
ya Kundi la waasi la FDLR.
masuala tete
Lakini masuala mengine yamesalia bila
kutatuliwa. Mfano, bado haijulikani serikali ya DRC itachukua hatua gani
kwa baadhi ya viongozi wa Kundi hilo la M23, ambao hawapati msamaha
kutokana na kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, ubakaji na uhalifu
wa kivita. Viongozi hao wameorodheshwa katika orodha ya jamii ya
kimataifa ya wahalifu wa kivita.
Miongoni mwa viongozi wa kundi hilo ambao
hawajapewa msamaha ni aliyekuwa kiongozi wao Askofu Runiga, Brg.
Jenerali Bouduain Ngaruye na Kanali Sultan Makenga na wengineo
Pia haijabainaka wazi hatma ya zaidi ya waasi wa zamani 1500 wa M23 waliojisalimisha nchini Uganda iwapo watarudi Congo au la.
No comments:
Post a Comment